Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, George Simbachawene amemtaka Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kutayarisha utaratibu wa motisha kwa fungu 25 na fungu 37 kwa Watumishi wanaojituma na kufanya kazi kwa bidii Ili kuhakikisha weledi na ufanisi wa kazi unaongezeka.
Simbachawene, ameyasema hayo hii leo Machi 14, 2023 jijini Dodoma, wakati akifungua mkutano wa kwanza wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Waziri Mkuu na kusema kuwa ushindanishaji huo uzingatie vigezo vitakavyowekwa kwa kada na ngazi za Watumishi au madaraka.
Amesema, “wajibu wa mabaraza haya kama vyombo vya ushauri na usimamizi ni kuhakikisha kuwa waajiri na watumishi wanatambua wajibu na haki zao, pia wanazingatia maadili ya utumishi wao ili kuleta matokeo ya utendaji wa kazi yenye tija, staha na upendo.”
Aidha, Simbachawene amebainisha kuwa, “Serikali imedhamiria kwa dhati,kuondoa uzembe na vitendo vyote vya rushwa mahala pa kazi. Hii ni pamoja na kubana matumizi yasiyo ya lazima ili kuongeza tija,”amesema Simbachawene
Hata hivyo, amesema madhumuni ya mkutano huo wa Baraza la Wafanyakazi ni kwa ajili ya Uwasilishaji wa Taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti ya Mwaka 2022/2023 na makadirio ya Bajeti ya mwaka 2023/2024.
“ukomo wa bajeti ya Fungu 37 – Ofisi ya Waziri Mkuu Sera umeongezeka kutoka shilingi bilioni 20.22 mwaka 2022/2023 hadi shilingi 23.47 mwaka wa fedha 2023/2024 sawa na ongezeko la asilimia 16.0,Ongezeko hilo ni wazi linalenga kuiongezea uwezo wa Ofisi kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi,” amebainisha Waziri huyo.