Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu itashiriki uzinduzi wa kuchangia Kampeni ya ‘GGM Kili Challenge 2022’, inayoratibiwa na Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGM) kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS).
Kampeni hiyo imelenga kuongeza nguvu na kasi ya mapambano dhidi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) kwa kuwashirikisha wadau na wananchi kwa ujumla.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Steven Kagaigai aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa tukio hilo la kuchangia Kampeni ya GGG Kili Challenge litazinduliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu), George Simbachawene, tarehe 14 Julai, 2022 katika Hoteli ya Weruweru River iliyopo Wilaya ya Hai.
Akizungumza jana na waandishi wa habari mkoani Kilimanjaro, Mkuu wa mkoa huo, Steven Kagaigai alisema harambee inatarajiwa kuzinduliwa tarehe 14 Julai, 2022 katika Hoteli ya Weruweru River iliyopo wilayani Hai mkoani humo.
Alisema uchangiaji wa fedha hizo unalenga zaidi jamii zilizoko kwenye mazingira hatarishi ya maambukizi ya VVU na kupunguza athari za UKIMWI.
Alisema kampeni hiyo hufanyika kila mwaka na ilianza rasmi tangu mwaka 2002 na huu ni katika mwendelezo wa ukusanyaji fedha kwa ajili ya mwitikio wa VVU na UKIMWI nchini sambamba na kutoa fursa ya utalii katika mlima Kilimanjaro.
“Shughuli kubwa katika siku hii ni kufanya harambee “Fund raising” ya uchangishaji fedha kutoka kwa wadau ambao watahudhuria tukio hilo. Tukio hilo litafuatiwa na tukio la kuwasindikiza wapanda mlima na waendesha baiskeli (Flag Off) siku ya pili yake tarehe 15 Julai 2022, katika Lango la Machame Halmashauri ya Wilaya ya Hai.
“Tarehe 21 Julai 2022 litafanyika tukio la kuwapokea wapanda mlima na waendesha baiskeli kuzunguka Mlima Kilimanjaro katika Lango la Mweka, Halmashauri ya Wilaya ya Moshi ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa George Simbachawene Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu),” alisema.
Mkuu huyo wa Mkoa aliongeza kuwa katika zoezi hilo litakaloambatana na kupanda mlima, huduma mbalimbali zitatolewa zikiwamo elimu na upimaji wa VVU, chanjo ya UVIKO – 19 pamoja na uchangiaji wa damu.
“Nawahamisisha wananchi wote kujitokeza kupata huduma hizi zitakazotolewa bila malipo. Pia wadau mbalimbali waliopo mkoani kwetu hata nje ya mkoa, makampuni, wafanyabiashara na wananchi wote kwa ujumla ndani na nje ya Mkoa wetu wanakaribishwa kujitokeza kwa wingi,” alisema Kagaigai.
“Nawasihi mjitokeze kwa wingi kupima na kujua afya zenu sambamba na kuchanja chanjo ya UVIKO 19 katika lango la Machame na Mweka kuanzia tarehe 15 Julai 2022,” aliongeza.
Akizungumzia zoezi la kupanda mlima, Meneja Mwandamizi anayehusika na ubia kutoka GGM, Manace Ndoroma alisema katika tukio hilo la upandaji wa Mlima Kilimanjaro, njia itakayotumika ni ile yenye changamoto nyingi “Njia ya Machame” ambayo imependekezwa mahsusi kuonesha jinsi mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI yalivyo na changamoto.
Naye Mkurugenzi Mkuu TACAIDS, Dk. Leonard Maboko amesema licha ya mafanikio yaliyofikiwa, UKIMWI bado ni tatizo nchini.
Alisema takwimu zinaonesha kuwapo kwa ongezeko la maambukizi mapya ya VVU hususan kwa makundi maalum yaliyo katika hatari kubwa ya maambukizi.
Alieleza kuwa hadi kufikia mwaka 2020 idadi ya watanzania wanaoishi na VVU imefikia watu 1,700,000 na maambukizo mapya kwa mwaka ni watu 68,000.
GGM Kili challenge ni mfuko ulioanzishwa mwaka 2002 na kampuni ya GGM. Kampeni hii inasimamiwa na GGM kwa kushirikiana na TACAIDS ikiwa na lengo la kukusanya fedha ili kuisaidia serikali ya Tanzania katika jitihada zake kufikia malengo ya sifuri tatu.
Malengo ya sifuri tatu yanamaanisha kupunguza kabisa kwa kufikia asilimia sifuri ya maambukizi mapya, sifuri ya unyanyapaa pamoja na sifuri katika vifo vitokanavyo na UKIMWI.