Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Simon Msuva, amesema kikosi chao kipo fiti kuwania alama tatu dhidi ya Niger, katika mchezo wa kwanza wa Kundi E wa kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2026.
Katika kundi hilo, Tanzania imepangwa na Morocco, Brazaville Zambia, Congo Niger. Taifa Stars itatupa karata yake ya kwanza dhidi ya Niger Jumamosi (Novemba 18) katika Uwanja wa Marrakech, Morocco.
Katika mchezo huo, Tanzania inahitaji alama tatu ili kujiweka katika nafasi nzuri kabla ya Jumanne (Novemba 21) kuikaribisha Morocco katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam.
Msuva amesema kuwa, kikosi chao kinaendelea na mazoezi na kila mchezaji yupo fiti kuipeperusha bendera ya taifa.
Nyota huyo anayekipiga JS Kabylie ya Algeria, amesema wachezaji wote wanatambua umuhimu wa mchezo huo, lengo lao ni kuvuna alama tatu ili kujiweka katika nafasi nzuri.
Msuva amekiri kuwa wapinzani wao wana timu nzuri yenye wachezaji bora, lakini Taifa Stars itafuata maelekezo ya benchi la ufundi na kuongeza juhudi zao binafsi kupata ushindi.
“Mara ya mwisho tulipocheza dhidi ya Niger tulishinda bao 1-0, tunakwenda kwao kuhakikisha tunapata alama tatu muhimu.
“Tumejiandaa kuhakikisha tunaipambania nchi yetu, kuitwa timu ya taifa ni kupewa heshima hivyo ni lazima kujituma, tunatambua umuhimu wa kupata ushindi katika mchezo huu,” amesema.
Nyota huyo amesema matokeo mazuri watakayopata katika mchezo huo, yatawapa matumaini ya kufanya vyema zaidi katika michezo mingine.
Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2026, zinatarajiwa kufanyika katika nchi tatu ambazo ni Marekani, Canada na Mexico.