Kiungo Mshambuliaji wa Tanzania Simon Msuva amewataka Mashabiki wa soka la Bongo kuondoa hofu dhidi yake kuhusu kukaa nje ya Uwanja wa kipindi kirefu.

Msuva kwa muda wa miezi kadhaa yupo jijini Dar es salaam, kutokana na changamoto kimaslahi iliopo kati yake na Uongozi wa klabu anayoitumikia Wydad Casablanca ya Morocco.

Akizungumzana Waandishi wa habari baada ya mchezo wa Kimataifa wa Kirafiki kati ya Tanzania ‘Taifa Stars’ dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, Msuva amesema hakuna haja kwa mashabiki kuwa na hofu, kwa sababu anaamini wakati wowote atapata nafasi ya kucheza kama ilivyokua zamani.

Amesema kwa sasa anafanya mazoezi binafsi akiwa jijini Dar es salaam ili kulinda kipaji chake kisishuke, na kama mambo yatamuendea vizuri kufuatia kesi iliopo kati yake na Wydad Casablanca huko FIFA, basi atarudi dimbani kupambana.

“Niwatoe hofu watanzania wasiwe na hofu kabisa na mimi, suala langu na Wydad Casablanca litakwisha na nitacheza tena soka kama ilivyokua zamani.”

“Kwa sasa ninafanya mazoezi binafsi na ndio maana nimeitwa kweye kikosi cha Taifa Stars, hivyo mambo sio mabaya.” amesema Msuva.

Msuva alikua sehemu ya kikosi cha Taifa Stars kilichocheza jana Jumatano (Machi 23) Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, huku akitoa pasi ya bao la tatu lililofungwa na George Mpole anayeitumikia klabu ya Geita Gold FC.

Mabao mengine ya Taifa Stars katika mchezo huo yalipachikwa wavuni na Dismas Novatus pamoja na Mbwana Ally Samatta.

Simon Msuva: Kwa Simba SC, Young Africans HAPANA
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Machi 24, 2022