Kiungo Mshambuliaji wa Tanzania Simon Msuva, amethibitisha kufuatwa na viongozi wa klabu za Simba SC na Young Africans SC, ili akubali kujiunga nazo kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Michuano ya Kimataifa.
Msuva ambaye kwa sasa ni mchezaji huru kufuatia kuachana na Mabingwa wa Soka Barani Afrika upande wa vilabu Wydad Casablanca, yupo nchini Tanzania kwa zaidi ya miezi mitatu akifanya mazoezi binafsi ya kujiweka ‘FIT’.
Kiungo huyo ambaye aliwahi kucheza Young Africans kabla ya kutimkia Morocco, amesema kwa nyakati tofauti viongozi wa klabu za Simba SC na Young Africans wamemfuata kumshawishi ili ajiunge nao kwa msimu ujao, lakini hadi sasa hajafanya maamuzi yoyote.
Hata hivyo Msuva amesema huenda akakubali kujiunga na moja ya timu hizo kubwa nchini Tanzania, hivyo amewataka Mashabiki wa soka nchini kuendelea kuwa na subra.
“Timu zote kubwa za hapa nchini zimenifuata kwa ajili ya mazungumzo ya kunisajili lakini bado sijafikia muafaka kwa kuwaomba wanipe muda . Kati ya timu hizo basi mojawapo huenda nikajiunga nayo.” Amesema Msuva
Mara ya mwisho Msuva alionekana Dimbani akiwa na kikosi cha Cambiaso Sports wakati wa mchezo wa Kirafiki dhidi ya Simba SC uliopigwa Mo Simba Arena, jijini Dar es salaam.
Katika mchezo huo Msuva aliifungia Cambiaso Sports mabao mawili, huku Simba SC ikiibuka na ushindi wa mabao matatu.