Kiungo Mshambuliaji Simon Msuva amewataka Watanzania kuwa na imani kubwa na timu yao ‘Taifa Stars’ kuelekea mchezo wa Kwanza wa kuwania kufuzu Fainali za Afrika ‘AFCON 2023’ dhidi ya Niger.
Taifa Stars imewasili nchini Benin tayari kwa mchezo huo utakaopigwa kesho Jumamosi (Juni 04) katika Uwanja wa taifa wa nchi hiyo (Stade de l’Amitie) ambao unatumiwa na timu ya taifa ya Niger kama uwanja wake wa nyumbani kufuatia Uwanja wa taifa wa nchi hiyo (Stade Seyni Kountché) kushindwa kufikia vigezo vya CAF.
Msuva amesema wachezaji wote wa Stars baada ya kuwasini Benin wapo katika hali nzuri na wana morari kubwa ya kupambana, hivyo amewaataka Watanzania kudumisha dua ya kuwaombea, ili wafanikishe lengo la kuondoka ugenini na alama tatu.
“Tuna Morari ya hali ya juu kama wachezaji, tunamshukuru mungu wachezaji wote ni wazima, hapa tulipokuja tumekuja kwa mara ya pili, kama mnakumbuka mara ya kwanza tulipata matokeo dhidi ya wenyeji halisi Benin kama mnakumbuka, ninaamini kesho tutakua na kumbukumbu ya ushindi tulioupata hapa, japo tutacheza na timu tofauti.”
“Wachezaji wanafahamu umuhimu wa huu mchezo, kwa sababu ndio mchezo wetu wa kwanza na inatulazimu kupambana ili tupate ushindi ambao utatusaidia katika kampeni yetu ya kuwania kufuzu AFCON 2023, tunawaomba watanzania watuombee ili tuweze kupambana na kupata matokeo mazuri tukiwa hapa ugenini.” amesema Msuva
Baada ya mchezo wa kesho Jumamosi (Juni 04), Stars itarejea jijini Dar es salaam kucheza mchezo wa Mzunguuko wa Pili wa Kundi F dhidi ya Algeria utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa Juni 08.