Hatimae mshambuliaji kutoka nchini Italia Simone Zaza amefanikiwa kuondoka magharibi mwa jijini London na kujiunga kwa mkopo na klabu ya Valencia ya nchini Hispania.
Zaza alikuwa na wakati mgumu wa kucheza katika kikosi cha kwanza cha West Ham Utd baada ya kusajiliwa kwa mkopo mwanzoni mwa msimu huu akitokea kwa mabingwa wa soka nchini kwao Italia Juventus.
Makubaliano ya uhamisho wake kuelekea West Ham Utd yalikua asajiliwe moja kwa moja endapo kiwango chake kingemridhisha meneja wa wagonga nyundo wa jijini London Slaven Bilic, lakini imekua tofauti.
Zaza amejiunga na Valencia na kazi kubwa inayomkabili kwa sasa ni kuhakikisha anaonyesha ushirikiano dhidi ya wachezaji wengine, ili kuinasua Valencia katika nafasi ya 17 kwenye msimamo wa ligi ya nchini Hispania (La Liga).
Inaaminika meneja wa klabu ya Valencia Salvador González Marco, atamuwezesha mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 25 kuchezeza katika kikosi cha kwanza ili kufanikisha azma ya kuondokana na mtihani wa kushuka daraja unaomkabili.
Valencia watalipa kiasi cha Pauni milioni 1.75 kama ada ya uhamisho wa mkopo wa Zaza, na kama wataridhishwa na uwezo wake watatakiwa kulipwa kiasi cha Pauni milioni 14.5 ili wamsajili moja kwa moja.