Hatimaye ile siku inayowaumiza kichwa Watanzania wengi wanaomiliki simu imewadia ambapo mbivu na mbichi zitajulikana leo majira ya saa sita usiku baada ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuzima simu zote feki nchini.

Kaimu Mkurugenzi  Mkuu wa TCRA, James Kilaba jana alisisitiza kuwa Mamlaka hiyo itatekeleza zoezi hilo leo kama ilivyokuwa imepangwa, yaani usiku wa leo kwani suala la usalama halijalishi idadi ya watu wanaomiliki simu.

Katika hatua nyingine, Kilaba aliwaonya mafundi simu na wauzaji wanaotumika kubadili nambari za utambuzi wa simu kuwa ni kosa kisheria na kwamba anayefanya hivyo atakabiliwa na adhabu kali ikiwa ni pamoja na kifungo kisichopungua miaka 10 jela.

“Nawakumbusha wauzaji wa vifaa vya mawasiliano vya mkononi na mafundi kuwa ni kosa kubadilisha namba tambulishi za vifaa vya simu za mkononi, kwani adhabu yake ni kifungo kisichozidi miaka kumi (10) au faini isiyopungua Sh millioni 30 au vyote kwa pamoja,” alisema Kilaba.

Mamlaka hiyo iliwataka mafundi simu wote kuhakikisha wamejiandikisha na kutambuliwa na kwamba watakaokuwa wanafanya kazi kwa kujificha watakabiliwa na adhabu kali.

Akifafanua kuhusu zoezi hilo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo alisema kuwa wenye simu feki wataona tu kuwa hawawezi kupiga wala kupokea simu lakini simu zao zitaendelea kuwa katika hali ya kawaida ikiwa ni pamoja na kuona majina yaliyoko kwenye kitabu cha nambari za mawasiliano (phone book) na mengine.

Ongezeko la ubakwaji na ulawiti kwa watoto laongezeka
Basi Kampuni ya Tahmeed lateketea kwa moto