Kocha wa viungo wa Singida Big Stars (SBS), Mussa Hamis amesema hali ya utimamu wa wachezaji wake imekamilika kwa asilimia kubwa huku kocha mkuu wa timu hiyo, Hans Van Pluijm akirejea mjini Singida kuendelea na maandalizi ya kuikabili Young Africans Mei 4.
SBS itaikaribisha Young Africans katika Uwanja wa CCM Liti, mjini Singida katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara Mei 04, kisha itaikabili tena timu hiyo kutoka Dar es salaam katika mpambano wa Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ Mei 07.
“Timu imekuwa nje ya uwanja kwa zaidi ya mwezi sasa tutakuwa na mchezo wa Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ dhidi ya Young Africans Mei 4 wachezaji wangu wapo fiti kwa asilimia 90 na wanaendelea na mazoezi ya uwanjani chini ya kocha Hans ambaye amerejea akitokea kumuozesha binti yake nchini Marekani.”
“Kazi yangu kama kocha wa viungo nimeifanya kwa usahihi na umakini ili kupunguza hari ya majeruhi na kuongeza kasi ya pumzi kwa wachezaji kwa kuwapa mazowezi ambayo yamewaweka timamu kwa asilimia kubwa,” amesema Hamis.
Katika hatua nyingine Hamis amesema Kocha Mkuu Pluijm amerejea muda sahihi hivyo anaamini atawapa mazoezi ya mbinu zaidi kiwanjani ili kuhakikisha wanaikabiri Young Africans kwa tahadhari na kupata matokeo ya ushindi.