Uongozi wa Klabu ya Singida Big Stars umeendelea kusisitiza hautokubali kumuachia Kiungo kutoka nchini Brazil Bruno Gomes, ambaye anahusishwa na Usajili wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans, mwishoni mwa msimu huu.

Mwenyekiti wa Singida Big Stars, Ibrahim Mirambo, amesema bado wana mipango na mchezaji huyo kwa ajili ya msimu ujao wa michuano Ligi Kuu Tanzania Bara na ile ya Kimataifa.

Amesema hawana mpango wa kumuuza nyota huyo kwa klabu yoyote na kwamba wanachohitaji ni kukiimarisha kikosi cha timu hiyo kuelekea msimu ujao ambao wanauhakika wa kushiriki michuano ya kimataifa.

Ameongeza kuwa, Bruno bado ana mkataba wa muda mrefu (miaka miwili) na hawana mpango wa kumuuza na ataendelea kusalia ndani ya kikosi cha Singida hadi hapo mkataba wake utakapofikia tamati.

Mirambo amesema wanapambana timu yao kufanya vizuri na kumaliza ligi katika nafasi ya tatu pamoja na kuhakikisha wanacheza fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho ‘ASFC’.

Singida Big Stars wako nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara wakiwa na alama 51, juu ya Azam FC ambao wako nafasi ya nne wakiwa na alama 50, Simba SC nafasi ya pili alama 63 na Young Africans ikiongoza msimamo kwa alama 68.

Katika michuano ya ASFC, Singida Big Stars wametinga Nusu Fainali na watakutana na Young Africans kwenye mchezo utakaopigwa Uwanja Liti mkoani, Singida nusu fainali nyingine ikiwakutanisha Simba na Azam FC katika Dimba la Nangwanda Sijaona lililopo Mtwara.

Ajali ya basi yauwa 11 wakitoka kwenye mazishi
Man City kumrudisha Jude Bellingham England