Uongozi wa Singida Big Stars umeendelea kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu uhalali wa Mshambuliaji kutoka DR Congo Fancy Kazadi Kasengu, ambaye amekuwa gumzo kwenye Michuano ya Kombe la Mapinduzi 2023.
Mshambuliaji huyo ambaye amewahi kucheza soka kwenye klabu za AS Vita, DC Motema Pembe (DR Congo) na Wydad Casablanca (Morocco), amekuwa akitajwa kama mchezaji ambaye anapita njia Singida Big Stars, huku lengo kuu ni kutimkia Young Africans.
Tetesi nyingine zinadai kuwa Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 30, yupo klabuni hapo kwa ajili ya kufanyiwa majaribio, kabla ya kusainiwa kwa ajili ya michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mwenyekiti Singida Big Stars Ibrahim Mirambo amesema wanasikia taarifa tofauti kuhusu Mshambuliaji Kazadi, lakini ukweli ni kwamba, Mchezaji huyo ni halali klabuni hapo.
Amesema Klabu yao haina utaratibu wa kuwafanyia majaribio wachezaji kama ilivyo kwa klabu nyingine za Tanzania, na katu haiwezi kutumika kama daraja la kumpeleka mchezaji kwenye klabu nyingine.
“Singida Big Stars hatuna utaratibu wa wachezaji kuja kufanya majaribio, kila mchezaji unaemuona amevaa jezi yetu ujue ameshasaini kwa maana hiyo taarifa zinazoenea kuwa Kazadi hajasaini Singida ni Uongo maana ni mchezaji wetu halali” amesema Mirambo
Kwa mara ya kwanza Kazadi ameonekana akiwa na jezi ya Singida Big Stars kwenye Michuano ya Kombe la Mapinduzi 2023 huko Kisiwani Unguja ‘Zanzibar’, na tayari ameshafunga amabo matano.
Bao moja akiifunga Young Africans katika mchezo wa Hatua ya Makundi uliomalizika kwa sare ya 1-1, mengine manne akiifunga Azam FC katika ushindi wa 4-1 uliopatikana juzi Jumapili (Januari 08), kwenye mchezo wa Nusu Fainali.