Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’ imezifungia kusajili klabu za Tanzania Prisons na Singida Big Stars zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kosa la kusajili wachezaji wenye mikataba na klabu zingine.
Uamuzi wa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji umefanywa kwa kuzingatia Kanuni ya 47 (21) ya Ligi Kuu, baada ya kuzikuta na kosa hilo. Adhabu hiyo ni kwa dirisha moja la usajili.
Tanzania Prisons ilimsajili Mlinda Lango Musa Mbise wa Coastal Union wakati ikifahamu kuwa bado ana mkataba na klabu hiyo.
Nayo Singida Big Stars ilimsainisha mkataba Mlinda Lango Metacha Mnata, huku akiwa bado ana mkataba na klabu ya Polisi Tanzania.
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji imezikumbusha klabu zote nchini kuwa usajili wa wachezaji unafanywa kwa kuzingatia kanuni, na kama zitakiuka kanuni zitachukuliwa hatua kwa mujibu wa kanuni.