Kikosi cha Singida Big Stars kimeweka kambi jijini Dar es salaam kikijiandaa na mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam FC, utakaopigwa Oktoba 03 katika Uwanja wa Azam Complex-Chamazi.
Timu hiyo inyoshiriki kwa mara ya kwanza Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2022/23, imedhamiria kupambana na kupata matokeo mazuri kwenye mchezo huo, ili kurekebisha makosa yaliyopelekea kupata sare ya 1-1 dhidi ya Geita Gold FC juma lililopita jijini Mwanza.
Msemaji wa Singida Big Stars Hussein Massanza amesema kikosi chao kimedhamiria kupambana kikamilifu dhidi ya Azam FC, huku wakiamini watapata alama tatu katika Uwanja wa ugenini.
“Tumedhamiria kuendelea kupambana katika michezo yetu ya Ligi Kuu, tumeanza vizuri sana japo katika mchezo uliopita tulipata matokeo ya sare dhidi ya Geita Gold FC, kikosi kitakua hapa kwa ajili ya kambi,”
“Tunajua Azam FC wana timu nzuri msimu huu, lakini tuna imani kubwa na kikosi chetu kitapambana katika uwanja wa ugenini, tunaamini utakua mchezo mgumu sana, lakini bado tunasisitiza lengo letu ni alama tatu.”
Singida Big Stars imekua ikivutia kikubwa kwa mashabiki wa Soka la Bongo msimu huu kutokana na uwepo wa mastaa wapya wa ndani na nje ya nchi ambao wamekuwa wakifanya vizuri chini ya kocha wa zamani wa Young Africans, Hans Pluijm.
Singida Big Stars inashika nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na alama nane, huku Young Africans ikiongoza msimamo huo kwa kufikisha alama 10 sawa na Simba SC iliyozidiwa mabao ya kufunga na kufungwa.