Afisa Habari wa Mtibwa Sugar Thobias Kifaru amesema ushindi wa jana Jumanne (Oktoba 18), dhidi ya Singida Big Stars, umedhihirisha kikosi chao kinajua kupambana na kutokuta tamaa.
Mtibwa Sugar ilishinda 1-0 katika Uwanja wake wa Nyumbani Manungu Complex Mkoani Morogoro, bao lao likifungwa na Mshambuliaji Charles Ilamfya katika kipindi cha pili.
Kifaru amesema waliiheshimu sana Singida Big Stars, kutokana na kuwa na kikosi kizuri na chenye wachezaji wenye uwezo mkubwa, lakini ukomavu na ukubwa wa Mtibwa Sugar katika Soka la Tanzania viliwabeba na kupata alama tatu muhimu baada ya dakika 90.
Hata hivyo Mkongwe huyo katika Tasnia ya usemaji, ametoa tahadhari kwa klabu nyingine za Ligi Kuu, akisema kwa yoyote atakaekutana na Mtibwa Sugar anapaswa kujiandaa kikamilifu la sivyo moto utamuwakia, huku akisisitiza wapo tayari kuikabili Dodoma Jiji FC kwenye mchezo unaofuata.
“Singida Big Stars wana nyota wengi sana ila sisi tumewadhihirishia tunajua, hili ni onyo kwa yeyote atakayeoita mbele, tunajiandaa kwenda Dodoma sasa,”
“Mtibwa Sugar inajua namna ya kucheza michezo yenye Presha, tulijua Singida Big Stars wangecheza vipi hapa kwetu, alichokifanya Kocha wetu Mayanga ni kuwatuliza wachezaji na kuwasisitiza watumie ukumbwa na uzoefu wao kushinda mchezo, na ndicho kilichotokea.” amesema Kifaru
Ushindi wa jana Jumanne (Oktoba 18), unaifanya Mtibwa Sugar kufikisha alama 12 zinazowapaisha hadi kwenye nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu, ikitanguliwa na Manguli Simba na Young Africans wenye alama 13 kila mmoja.