Benchi la ufundi la Singida Fountain Gate, limefichua kuwa ushindi wa mabao 3-2 iliyoupata dhidi ya Namungo FC, umeongeza morali ya kikosi chao katika maandalizi ya mchezo dhidi ya Young Africans.
Singida itachuana na Young Africans ljumaa (Oktoba 27) katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Timu hiyo itaingia katika mchezo na Young Africans ikiwa na kumbukumbu ya kupata ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Namungo FC, katika Uwanja wa Majaliwa mjini Ruangwa, mwishoni mwa juma lililopita.
Kocha msaidizi wa Singida FG, Thabo Senong amesema ushindi huo umekipa nguvu kikosi chake kujiandaa vyema kwa mchezo huo mgumu.
Kocha huyo amekiri kuwa, Young Africans ni timu ngumu na kubwa lakini benchi la ufundi linaendelea kuwanoa vyema wachezaji kupata ushindi mnono.
“Najua Young Africans ina kikosi kizuri, lakini hata sisi tuna timu nzuri zaidi, tumetoka kushinda dhidi ya Namungo FC ambao wana kikosi bora, ushindi huo umetuongezea nguvu zaidi na naamini tutashinda,” amesema.
Kocha huyo amesema nia yao ni kushinda kila mechi ili kumaliza katika nafasi nne za juu.
Katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Singida ipo nafasi ya saba ikiwa na alama nane baada ya kushuka dimbani mara sita.
Timu hiyo imeshinda mechi mbili, imetoka sare mara mbili na imefungwa michezo miwili.