Klabu ya Singida Fountain Gate FC imekutana na rungu lingine la kufungiwa kusajili, baada ya kuthibitika inadaiwa na aliyekuwa mchezaji wao kutoka nchini Brazil Rodrigo Figueiredo Carvalho.
Hatua hiyo imekuja ikiwa ni siku kadhaa klabu hiyo kutakiwa kumlipa Beki kutoka nchini Ivory Coast Serge Pascal Wawa ambaye alishinda kesi ya malipo ya malimbikizo ya mishahara.
Taarifa iliyotolewa leo Jumatatu (Desemba 11) na SHirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’ imeeleza kuwa uamuzi huo umefanywa na Shirikisho la soka Duniani ‘FIFA’ baada ya Carvalho kushinda kesi ya madai dhidi ya klabu hiyo, inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mchezaji huyo alifungua kesi FIFA akidai malipo ya malimbikizo ya mishahara.
FIFA iliitaka Singida Fountain Gate FC kumlipa Rodrigo Figueiredo Carvalho ndani ya siku 45 tangu uamuzi huo ulipotolewa, lakini haikutekeleza hukumu hiyo.
Wakati FIFA imeifungia klabu hiyo kufanya uhamisho wa wachezaji kimataifa, Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’ limeifungia kufanya uhamisho wa ndani.
Hata hivyo TFF imezitaka klabu kuheshimu mikataba ambayo zimeingia na wachezaji pamoja na makocha ili kuepuka adhabu mbalimbali ikiwemo kufungiwa kusajili.