Singida Fountain Gate ikiwa chini ya benchi jipya la ufundi linaloongozwa na Kocha Mkuu Emst Middendorp, imeweka kambi fupi jijini Dar es salaam na kucheza mechi mbili za kirafiki kujiandaa kuikabili Future FC ya Misri, katika mchezo wa Raundi ya Kwanza wa michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Mchezo kati ya Singida na Future unatarajiwa kuchezwa Septemba 17 Uwanja wa Azam Complex, Dar es salaam huo ukiwa mtihani wa kwanza kwa benchi hilo jipya la ufundi.
Msemaji wa Singida Fountain Gate, Hussein Massanza amesema wameona wailete timu Dar es salaam ili kuzoea hali ya hewa na kulipa nafasi benchi lao jipya la ufundi kukiandaa kikosi chao kwa ajili ya mchezo huo wa Kombe la Shirikisho ili kuhakikisha wanashinda.
Kiongozi huyo amesema wamekuja Dar es Salaam na wachezaji wao wote lengo ni kutoa nafasi kwa benchi lao la ufundi kuwajua wachezaji na kuandaa mpango kazi kwa ajili ya mechi za mashindano ya Kimataifa na Ligi Kuu Tanzania Bara.
Amesema wanaimani kubwa na benchi lao jipya hivyo na wao kama viongozi watapambana kuhakikisha wanatimiza mahitaji yote ili kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye mashindano yote wanayoshiriki msimu huu.
Juma lililopita Singida Fountain Gate ililifuta kazi benchi la ufundi lililokuwa chini ya Kocha Mkuu, Hans Pluijm kutokana mwenendo wa kusuasua kwenye Ligi Kuu kufuatia kupata matokeo ya sare katika mechi mbili za awali walizocheza uwanja wa nyumbani CCM Liti.