Uongozi wa Singida Fountain Gate umetoa sababu za kutokwenda Tunisia kuweka kambi ya maandalizi ya msimu ujao wa mashindano, na badala yake timu hiyo itajichimbia mkoani Arusha.

Timu hiyo itakayoshiriki mechi za Ngao ya Jamii, Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ na Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu ujao 2023/24, ilikuwa iondoke nchini Julai 15, ila uongozi umesema hawataenda tena licha ya kwamba walipata ofa kutoka US Monastir waliingia nao mkataba wa ushirikiano katika masuala ya utawala, uendeshaji na ufundi.

Afisa Habari wa Singida Fountain Gate, Hussein Masanza amesema kutokana na kutokuwa na muda wa kutosha wameamua kuweka kambi Arusha kutokana na kuwa na mambo mengi lakini wakiwa na muda mchache mno iwapo watasafiri nje ya nchi.

“Tuna Singida Day tuliyopanga kuifanya mapema mwezi ujao, Ngao ya Jamii itakayochezwa Tanga na ishu za usajili bado hatujakamilisha, hivyo muda kwetu ni mchache ndio maana uongozi umeamua tubaki hapa hapa lengo likiwa ni kujiweka fiti kwa kuanza mandalizi mapema,” amesema.

“Kambi ya Arusha itaanza Julai 10 lengo ni kuona tunakamiliasha mipango ya usajili na kuungana pamoja kwaajili ya kujiweka tayari kwaajili ya ushindani msimu ujao,” amesema Massanza na kuongeza wamewasiliana na wenyeji wao Monastir ili kuwajulisha kuwa hawataenda tena.

“Kama mambo yatakwenda vizuri watatafuta mechi za kirafiki Kenya na Uganda ili kujipima uwezo na kujiweka tayari kwa msimu mwingine mpya na tayari wachezaji wamejulishwa wanatakiwa kukutana Jumapili tayari kwa safari hiyo ya Arusha na kambi ikiisha wanarudi Singida,” amesema.

CHENETA yachekelea msaada BMT
Malisa akata mzizi wa fitna kero za Wananchi