Mshauri wa Benchi la Ufundi la Singida Fountain Gate, Christopher Hughton amesema kama wachezaji na Benchi la Ufundi watazitumia vizuri siku watakazoweka kambi kujiandaa msimu ujao wa Ligi Kuu na mashindano ya kimataifa, wanayo nafasi ya kutwaa ubingwa.
Timu hiyo inatarajia kuelekea Tunisia juma lijalo kwa ajili ya kuweka kambi ya majuma matatu kujiandaa na msimu mpya wa mashindano ikiwemo Kombe la Shirikisho Barani Afrika, watakayoshiriki baada ya kumaliza nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu msimu uliopita.
Akizungumza mshauri huyo ameeleza kuwa maboresho ambayo wameyafanya ikiwemo usajili umekifanya kikosi hicho kuwa bora zaidi jambo ambalo linampa matumaini ya kutoa ushindani na kubeba mataji.
“Tumesajili wachezaji wenye uwezo mkubwa lakini kingine kizuri ni kubakisha wachezaji wetu muhimu ndani ya timu, hicho ni miongoni mwa vitu muhimu ambavyo vinaweza kutufanya kuwa bora zaidi,” amesema Hughton.
Aidha, kocha mkuu wa timu hiyo, Hans Pluijm alieleza kuwa tayari wachezaji wameanza kurejea nchini kwa ajili ya kuanza kambi ya siku chache kabla ya kuelekea Tunisia kwa ajili ya kambi hiyo.
Amesema yeye na wasaidizi wake watahakikisha wanajenga timu ya ushindani.