Kikosi cha wachezaji 23 cha Singida Big Stars kimeelekea Cairo, Misri tayari kwa mchezo wao wa Mkondo wa Pili wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Future FC, utakaopigwa Oktoba Mosi, mwaka huu.
Timu hiyo itavaana na Future FC kuwania kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo, itakayoanza majira ya saa 12 jioni kwenye Uwanja wa Al-Salam, Cairo.
Singida itaingia uwanjarni ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa bao 1-0 kwenye mechi ya awali iliyopigwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es salaam.
Ofisa Habari wa Singida, Hussein Masanza ameeleza kuwa benchi la ufundi chini ya Mathias Lule linaamini juu ya maandalizi ya kikosi hicho kuelekea mchezo huo wakiwa tayari kutafuta matokeo ugenini.
“Tunataka kumaliza tulichokianza Dar es salaam kwa hiyo kiujumla maandalizi yalikuwa makubwa na kocha ana imani kubwa na kikosi kwa ajili ya kuhakikisha tunatafuta matokeo na tunasonga hatua inayofuata,” amesema Masanza.
Singida wanaoshiriki kwa mara ya kwanza michuano hiyo walitinga raundi ya kwanza baada ya kuwatoa JKU ya Zanzibar kwa jumla ya mabao 4-3 ambapo kwenye mchezo wa kwanza waliibuka na ushindi wa mabao 4-1 kabla ya kuja kufungwa mabao 2-0.