Uongozi wa timu ya Singida Fountain Gate umesema unafikiria kumualika Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgeni rasmi katika mchezo wao wa raundi ya kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Future FC ya Misri utakaochezwa Jumapili (Septemba 17) katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es salaam.
Akizungumza na Azam Media, msemaji wa timu hiyo, Hussein Massanza amesema mazungumzo yanaendelea ili kuona kama maombi yao yatafanikiwa kwa raia huyo namba moja kuwepo uwanjani ili kuwapa sapoti wachezaji wao na kupata ushindi mnono utakaoamsha matumaini ya kutinga hatua ya makundi.
Msemaji huyo amesema wamedhamiria jambo hilo liwe la kitaifa kwa kutaka kuwaruhusu mashabiki kuingia bure uwanjani ili kuishangilia timu hiyo waweze kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania kwenye michuano hiyo ya kimataifa.
Massanza amesema katika mchezo huo, Singida itakuwa inaunganisha wananchi wote hivyo wanatarajia kuiunganisha nchi kupitia mchezo huo na kuweka pembeni tofauti zao za kishabiki na hatarajii kuona shabiki wa Tanzania akiwashangilia wapinzani wao Future FC.
“Dhamira yetu ni ushindi na tutafanya kila linalowezekana ili kupata ushindi ikiwemo kuwashirikisha viongozi wa serikali na watu mbalimbali kwa ajili ya mchango wao wa kimawazo ikiwemo klabu za Simba SC na Young Africans ambazo zina uzoefu ili pointi tatu tuzibakishe hapa nyumbani,” amesema Massanza.
Msemaji huyo amesema maandalizi yao kuelekea mchezo huo yanakwenda vizuri na Kocha wao mkuu, Ermst Middendorp ameahidi kuanza vizuri kibarua chake kutokana na utayari wa wachezaji wake.