Uongozi wa Singida Fountain Gate FC umeendeleza harakati za usajili na sasa unaelezwa kukamilisha uhamisho wa beki wa kulia, Kelvin Kijiri aliyekuwa anacheza katika kikosi cha KMC FC.

Imefahamika kuwa bosi wa juu katika timu hiyo alimtafuta Kijiri wakati KMC FC ikiwa imeweka kambi kwa ajili ya mechi mbili za mwisho za Ligi Kuu Bara jijini Mbeya.

Bosi huyo alifanya mazungumzo na kitasa huyo kisha walikuwa kusubiri hatima ya timu hiyo ambayo ililazimika kujiokoa kutoshuka daraja baada ya kushinda mchezo wa pili wa mtoano (Play Off) dhidi ya Mbeya City.

Baada ya kuwa sehemu ya wachezaji walioibakisha KMC FC kwenye Ligi Kuu, kigogo huyo alimpa mkataba Kijiri wa miaka miwili kuitumikia Singida Fountain Gate katika msimu ujao.

Baada ya Kijiri kuondoka, mabosi wa KMC kwa sasa wanahaha kutafuta mbadala wa mchezaji huyo kwa ajili ya kuongeza nguvu msimu ujao katika ligi ambayo inayotarajiwa kuwa na ushindani zaidi.

“Kijiri ameondoka KMC FC amejiunga na Singida, pengo lake tunaliziba siku sio nyingi ili tusitetereke kabisa kwenye kikosi chetu. Wapo wachezaji ambao tayari tumeanza nao mazungumzo,” kimesema chanzo cha ndani kutoka KMC.

Timu hiyo tayari imeanza mazungumzo na beki wa zamani Mbeya City, Kenneth Kunambi kwa ajili ya kupata huduma yake msimu ujao.

Hata hivyo, uongozi pia tayari umekwishamalizana na baadhi ya wachezaji wakiwamo Baraka Majogoro na Cliff Buyoya.

Vidokezo vya kujilinda wakati wa hatari, dharura
Maboresho Biashara ya Kaboni yaanza