Mbunge wa Singida Mjini, Mohamed Dewji ametangaza kutogembea tena nafasi hiyo ya ubunge katika uchaguzi mkuu utaofanyika Oktoba mwaka huu.

Dewji aliweka wazi uamuzi wake wakati akihutubia umati wa wananchi wa jimbo lake jana (Julai 8) katika uwanja wa ‘People’s Ground’ mjini Singida.

“Kwa kutambua heshima kubwa mlionipa na imani kubwa mlionionesha kwa vipindi vyote vya uongozi wangu kwa wanasingida wenzangu, ninawaomba sana mwaka huu nisigombee,” alisema Dewji.

Kauli hiyo ilizua simanzi kwa wananchi waliohudhuria ambapo baadhi yao walisikika wakipaza sauti ‘hapana… hapana’, wakimsihi mbunge wao huyo kutoliachia jimbo.

Hata hivyo, Dewji aliendelea na msimamo wake huku akiwasihi wananchi hao kutokuwa na wasiwasi kwa kuwa hakuwa analisaidia jimbo hilo kwa sababu yeye ni mbunge bali ni kutokana na uhalisia kuwa yeye ni mzawa wa Singida.

“Kinachonifanya niwaambie hiki ni kwa sababu nataka mfahamu kuwa dhamira yangu kwenu wananchi wangu haitokani na nafasi yangu kama Mbunge ama mwanasiasa. Dhamira yangu ni ya uzaliwa, dhamira yangu inatokana na mapenzi niliyonayo kwenu na imani niliyonayo juu ya uwezo wetu wa kuijenga Singida,” alisema.
Mbunge huyo kijana ambaye jarida la Forbes lilimtaja kuwa mmoja wa matajiri wakubwa Afrika, alitaja baadhi ya maendeleo aliyoyafanya Singida kwa ushirikiano wa wananchi hao.

Alisema wakati anaanza ubunge kulikuwa na shule mbili tu, lakini hadi sasa jimbo hilo lina shule 15 zilizojengwa kwa msaada wa mbunge huyo na wananchi. Pia wameweza kulipa ada kwa wanafunzi 15,000 na kutoa vyandarua 6000 kwa akina mama wajawazito na watoto na hivyo kupunguza vifo vya mama na mtoto kwa asilimia 50. Mo Dewji pia aliwapeleka madaktari bingwa jimboni hapo ambao waliofanya upasuaji wa ‘mtoto wa jicho’ kwa wananchi zaidi ya 1000.

Klitschko Awachokoza mabondia wa Uingereza
Sterling Aeleza Sababu Ya Kutohudhuria Mazoezi Ya Liverpool