Tanzania itaungana na nchi wanachama wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), katika kuadhimisha siku ya Chakula Duniani ambapo Kitaifa yanatarajiwa kufanyika mkoani Singida Oktoba 10 mwaka huu.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi ameyasema haya leo mjini Singida wakati akiongea na waandishi wa habari na kuongeza kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo anatarajiwa kuwa Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga.

“Mkoa wa Singida umepewa heshima na Taifa kuwa mwenyeji wa siku ya chakula Duniani na maadhimisho haya yatazinduliwa kesho hivyo wananchi wa Singida na mikoa jirani wajitokeze kwa wingi kwenye Uwanja wa Bombadia kuanzia kesho hadi tutapofikia kilele chake Oktoba 16, 2019,” amesema Bi. Nchimbi.

Amesema Takwimu za Wizara ya Kilimo zinaonyesha hali ya upatikanaji chakula kwa mwaka 2019/2020 ni nzuri kwani kiwango cha utoshelevu wa chakula ni asilimia 119 na uzalishaji wa mazao ya chakula ulifikia tani milioni.16,408,309 ukilinganisha na mahitaji ambayo ni tani milioni 13,842,536. 

Mkuu huyo wa Mkoa amefafanua kuwa kati ya hizo Tani milioni 9,007,909 ni mazao ya nafaka na tani milioni 7,400,400 ni mazao yasiyonafaka na kuwapongeza Watanzania kwa kutekeleza kauli mbiu ya maadhimisho hayo kwa vitendo.

“Kaulimbiu ya maadhimisho haya inasema (Lishe Bora kwa Ulimwengu Usio na Njaa) na inalenga kuhamasisha jamii na wadau wote wa sekta kilimo kuchangia katika kuhakikisha nchi yetu na dunia nzima inakuwa na chakula cha kutosha,” ameongeza Mkuu huyo wa Mkoa wa Singida Rehema Nchimbi.

Wananchi wa Itulike na Maheve Mjini Njombe wajipanga kupokea umeme
Mfumuko wa bei wa Taifa washuka