Klabu ya Singida United imetamba kuendeleza ubabe dhidi ya Young Africans katika mchezo wa ligi kuu ya soka Tanzania bara, utakaochezwa leo jioni Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Singida wametoa tambo hizo kupitia kwa Mkurugenzi wake Festo Sanga amesema wao na Young Africans hawana undugu wala urafiki kama ambavyo wengi wanadhani, na kudhirihisha hilo, ni kuibwaga katika mchezo huo bila kujali kuwa wapo kwenye mbio za ubingwa.
Amesema Singida United wanafahamu kuwa Young Africans wana hasira na timu yao kwa kuwa waliwafunga kwenye mchezo war obo fainali wa kombe la shirikisho la soka (ASFC), uliopigwa Aprili Mosi mwaka huu kwenye dimba la Namfua, mjini Singida.
Hata hivyo Katibu Mkuu wa Young Africans, Charles Boniface Mkwasa amesema Singida hukamia sana timu yao pindi wanapokutana, tofauti na na inavyokua kwa timu nyingine, huku akitolea mfano mchezo dhidi ya mtuibwa ambao waliwabanjua vijana hao wa Namfua mabao matatu juma lililopita.
Akijibu hoja ya kuwakamia Young Africans, Sanga amesema ni kweli huwa wanafanya hivyo, na wao sio timu ya kwanza duniani kuikamia timu pinzani. Amesema hata Young Africans wanapokutana na mahasimu wao Simba SC huwa wanakamia.
Katika mchezo wa mzunguuko wa kwanza ligi kuu ya soka Tanzania bara uliozikutanisha Young Africans na Singida Utd kwenye uwanja wa Namfua mjini Singida, timu hizo zilikwenda sare ya bila kufungana.