Singida United haitaki masikhara kabisa na mechi zilizoko mbele yake kwani kocha wake, Hans Van Pluijm amefichua kuwa baada ya kuondoshwa kwenye kombe la Mapinduzi, akili zake sasa ni kwenye mchezo unaokuja dhidi ya vinara wa Ligi Kuu Bara, Simba.

Pluijm alisema mashindano ya Mapinduzi yalikuwa mazuri na anajivunia kiwango ambacho wachezaji wake wameonyesha licha ya kuwa ndio mara yao ya kwanza kushiriki. Singida ilifungwa bao 1-0 na Azam kwenye mchezo wa nusu fainali.

“Mashindano ni mazuri na kufika katika hatua ya nusu fainali ni kitu kikubwa kwetu kwani inaonyesha jinsi gani tunazidi kuimarika, tumeyachukua pia mashindano haya kama maandalizi ya mechi za ligi kuu,” alisema Pluijm.

“Changamoto ambayo ilikuwa kwetu ni kucheza mechi nyingi kwa kipindi kifupi jambo ambalo lilikuwa linapunguza uwezo wa wachezaji wangu,” alisisitiza.

“Tunacheza mechi ijayo na Simba katika ligi, ni timu ngumu yenye wachezaji wazuri, tunaanza maandalizi mapema ili kupata matokeo ya ushindi,” alisema kocha huyo wa zamani wa Yanga.

 

Mrema afungua kesi rasmi dhidi ya kuzushiwa kifo
Sababu ya Ronaldo kushika namba 49 duniani