Mabingwa wa Soka nchini Ufaransa PARIS Saint-Germain ‘PSG’ wameripotiwa wako tayari kuachana na mastaa wao Neymar na Lionel Messi utakapofika mwisho wa msimu huu 2022/23.
Taarifa kutoka jijini Paris zimeripoti kuwa, kikosi cha PSG kitajengwa upya na inaaminika wachezaji saba tu wameorodheshwa ambao watabaki, lakini mastaa hao wawili hawakujumuishwa kwenye kikosi hicho huku Kylian Mbappe akiongoza katika orodha hiyo.
Imeelezwa kuwa PSG ina mkakati wa kufanya mabadiliko makubwa msimu huu utakapomalizika, huku ikijiandaa kuachana na Messi ambaye mkataba wake unamalizika hivi karibuni.
Inaaminika kwamba PSG ilikuwa tayari kumwongeza mkataba mpya Messi lakini staa huyo amesuasua na anataka kufahamu malengo ya klabu hiyo msimu ujao.
Messi amehusishwa na klabu yake ya zamani ya Barcelona na Inter Miami inayomilikiwa na David Beckham, huku taarifa zikiripoti nyota huyo wa kimataifa wa Argentina anataka kumalizia soka lake Ulaya.
Hivi karibuni mashabiki wa FC Barcelona wamemuimba Messi wakati mchezo wao wa El Classico dhidi ya Real Madrid na kuzidisha uvumi wa kwamba fundi huyo huenda akarejea tena Nou Camp, Messi mwenye umri wa miaka 35, amekuwa akihusishwa sana kuwa kwenye mpango wa kutaka kuondoka PSG mwezi Juni ambapo mkataba wake wa sasa unamalizika.
Juma lililopita ziliibuka ripoti kuwa FC Barcelona wamefanya mawasiliano na wawakilishi Messi kumshawishi afikirie kurudi nyumbani kwa msimu ujao.