Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) limebadilisha jina la Michuano yake mapya, lakini Rais, Patrice Motsepe amesisitiza yatakuwa na neema kubwa ya mkwanja, huku Simba SC ikiwa mshiriki pekee kutoka ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ‘CECAFA’.
Awali Michuano hiyo ambayo pendekezo la awali ni kushirikisha timu nane, yanayoanza Oktoba yalipangwa kuitwa Super League lakini sasa yatajulikana kama African Footbal League (Ligi ya Soka ya Afrika).
“Marafiki zetu wa Ulaya walitushauri kutotumia jina la ‘Super League’ kutokana na uhusiano mbaya na ile ya kwao ilivyofeli miaka iliyopita,” alisema.
Motsepe ameeleza michuano hiyo itashirikisha timu nane pekee, zikiwemo timu zilizofuzu Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2023 Ahly ya Misri, Wydad Casablanca ya Morocco, Esperance ya Tunisia, na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
Nyingine ni TP Mazembe ya DR Congo, Enyimba ya Nigeria, Simba SC ya Tanzania na Petro Atletico ya Angola.
“Tumeamua kubadilisha jina la Super League kuwa Ligi ya Soka ya Afrika,” Motsepe alisema katika mahojiano na Televisheni ya beIN Sport ya Qattar.
“Ligi ya Soka ya Afrika itaanza Oktoba kama ilivyopangwa, itakuwa ligi bora zaidi kutokana na ukubwa wa zawadi,” alisema Motsepe na kuongeza maelezo zaidi ya michuano hiyo itafafanuliwa hivi karibuni Ivory Coast.
Bingwa wa michuano hiyo atapewa 28 bilioni. Klabu zitatoka katika kanda tatu za Afrika ambazo ni Kaskazini, Kati/Magharibi, Kusini/ Mashariki.