Sir Alex Ferguson amesema Manchester United haikukosea kumteua David Moyes kuwa mrithi wake kama meneja wa klabu hiyo.

Ferguson alitetea uteuzi wa mkufunzi huyo wa zamani wa Everton, aliyefutwa kazi na United baada ya kuhudumu miezi minane tu, kwenye makala kwa jina Secrets of Success (Siri ya Ufanisi) ambayo itaonyeshwa kwenye runinga ya BBC One Jumapili.

“Tulifanya kadiri ya uwezo wetu katika hali iliyokuwepo,” Ferguson mwenye umri wa miaka 73, amemwambia mwandishi wa BBC Nick Robinson, aliyeandaa makala hiyo.

“Tulimchagua mtu aliyefaa.”

Ferguson alihitimisha ukufunzi wake wa miaka 26 United mwaka 2013, na kumpendekeza raia mwenzake wa Scotland David Moyes kuwa mrithi wake.

Alimwambia tu afisa mkuu mtendaji wa klabu hiyo David Gill kuhusu mpango wa kustaafu miezi kadha mapema na anadai wengi wa watu ambao walifaa Zaidi kumrithi hawangepatikana.

“Sidhani tulifanya kosa kamwe. Ninafikiri tulimchagua mtu aliyefaa,” Ferguson anasema. “Kwa bahati mbaya, mambo hayakumuendea vyema David.

“Jose Mourinho alikuwa anarejea Chelsea, Carlo Ancelotti alikuwa anarudi Real Madrid, Jurgen Klopp alikuwa ametia saini mkataba na Dortmund, Louis van Gaal naye alikuwa anasalia na Uholanzi kwa Kombe la Dunia.”

Ferguson pia amemwambia Robinson, kwamba Moyes huenda hangeliteuliwa iwapo winga wa zamani wa United Ryan Giggs hangeliamua kuendelea kucheza hata baada ya kutimiza miaka 40.

Giggs, aliyechezea klabu hiyo mechi 963, alisimamia mechi nne baada ya Moyes kufutwa na ndiye msaidizi wa meneja wa sasa Louis van Gaal.

“Iwapo Ryan Giggs angelikuwa amestaafu, tuseme akiwa na miaka 35, kuna uwezekano mkubwa ningekuwa nimemteua msaidizi wangu,” anasema Ferguson.

“Na huenda angeingia kwenye kazi hiyo sawa na anavyofanya sasa akiwa na Louis van Gaal.”

Van Gaal amesema Giggs atakuwa meneja wa United baada yake kuondoka, jambo ambalo klabu hiyo haijathibitisha wala kukanusha.

Yametimia! Mkwasa Bosi Wa Ukweli Kweli Stars
David Moyes Akataa Kurejea England