Ushindi wa Umeya wa Halmashauri za Manispaa ya Ilala na Kinondoni umebainika kuwa ulibebwa na mbinu ya kipekee ya kutumia kalamu zilizowagharimu shilingi milioni 30.

Taarifa zilizothibitishwa na Ukawa zimeeleza kuwa umoja huo ulitoa kalamu maalum za kupigia kura ambazo zilikuwa na kamera maalum iliyokuwa inachukua taarifa za madiwani wake waliokuwa wanapiga kura na kuzituma kwa mtu maalum aliyeteuliwa kufuatilia zoezi hilo.

Mbunge wa Kawe, Halima Mdee alithibitisha kutumia mbinu hiyo akidai kuwa umoja huo uliamua kufanya hivyo baada ya kubaini mbinu chafu ya harufu ya rushwa iliyotanda ambapo walipata taarifa kuwa kuna baadhi ya wajumbe wao waliahidiwa rushwa ili wasiliti.

“Kama nilivyosema, kalamu zile ukizifungua tu ndani kuna kamera. Ukianza kuitumia kuna mtu maalum aliyetayarishwa kwa ajili ya kuangalia wajumbe wote wa Ukawa wanaopiga kura,” Mdee aliliambia gazeti la Mwananchi.

Mdee alieleza kuwa hiyo ilitokana pia na kitendo cha madiwani wawili wa Ukawa kuwasaliti wenzao katika zoezi la upigaji kura katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke.

“Wana Kinondoni wangetushangaa kama tungepata Umeya kwa idadi ya Madiwani waliotupatia. Kuna wajumbe mnakubaliana vizuri, lakini wakifika kwenye sanduku la kura wanabadilika. Kalamu hizi zimetusaidia sana kwa sababu tulikuwa 38, CCM walikuwa 20, na tumepata kura zilizopigwa kama tulivyotarajia,” alisema Mdee.

Alisema kuwa wapo wajumbe ambao walipokea fedha lakini walipiga kura zao kwa kutimiza wajibu wao kama madiwani wa Ukawa hivyo hilo ni fundisho kwa wote.

Katika hatua nyingine, Mdee alisema kuwa Umoja huo una uhakika wa kushinda nafasi ya Umeya wa jiji la Dar es Salaam katika uchaguzi utakaofanyika Jumamosi hii na kwamba watatumia mbinu tofauti na bora zaidi.

“Kwenye Umeya wa jiji tutakuja na njia tofauti. Hizi tulizozitumia kwenye Manispaa ya Ilala na Kinondoni tutaziboresha na tuna uhakika wa kuchukua Umeya wa jiji la Dar es Salaam,” anakaririwa Mbunge huyo wa Kinondoni ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha).

Katika uchaguzi uliopita, Boniface Jacob (Chadema) alishinda Umeya wa Kinondoni kwa kupata kura 38 dhidi ya kura 20 alizopata Benjamini Sitta wa CCM, huku nafasi ya unaibu Meya ukienda kwa Jumanne Mbunju (CUF).

 

Naye Charles Kuyeko (Chadema), alishinda nafasi ya Umeya wa Ilala kwa kupata kura 31 na nafasi ya Unaibu ilienda kwa Omari Kumbilamoto.

Brendan Rodgers Amtabiria Makubwa Mtukutu Suarez
Mahakama yafuta kesi dhidi ya kafulila