Zikiwa zimebaki siku 15 watanzania kufanya tukio la kihistoria la kumchagua rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, wabunge na madiwani, matukio yasiyotegemewa yanazidi kuripotiwa huku ushindani mkubwa ukiwa unaonekana na inazidi kuwa vigumu kumtabiri mshindi hasa wa nafasi ya urais.

Katika hali ambayo wengi hawakuitegemea, jana mgombea ubunge wa jimbo la Vunjo ambaye pia ni mwenyekiti wa TLP, Augustino Mrema aliungana na msafara wa mgombea urais kupitia CCM, Dk. John Magufuli na kuwataka wananchi wa jimbo hilo wampigie kura mgombea huyo wa CCM ingawa chama chake pia kimemsimamisha mgombea urais.

Katika kile kilichoonekana kama kulipa fadhira, Dk. Magufuli pia alimnadi Mrema na kuwataka wananchi kumpigia kura endapo wataona hawamtaki mgombea ubunge wa CCM, kuliko kufanya vinginevyo.

Augustine Mrema

“Ninampigia kampeni Innocent [Shirima], lakini kama hamumtaki Innocent ni heri mpeni angalau Mrema, msije mkapeleka mahali pengine,” alisema Magufuli.

Urafiki wa kushangaza wa kisiasa wa Magufuli na Mrema unatokana na mambo kadhaa, lakini haya ni baadhi ya mambo hayo.

Mwaka 2010, tunakumbuka Mrema alikutana na ushindani mkubwa katika jimbo la Vunjo na akaamua kuweka mambo hadharani alipokuwa bungeni ambapo alimuomba rais Jakaya Kikwete na CCM kwa ujumla wamsaidie, ingawa chama hicho pia kilikuwa kimemsimamisha mgombea ubunge jimboni humo.

Ingawa hakuna ushahidi wa moja kwa moja, hali ilionesha kuwa ombi la Mrema lilikubaliwa na CCM ambao walilegeza ushindani jimboni humo, hali iliyomuwezesha kushinda na kuwa wa kwanza kujitangaza alipofanya mahojiano na BBC mwaka huo.

Mgombea wa CCM aliyeshindwa katika jimbo hilo alipewa nafasi nyingine ya Ukuu Wa Wilaya, hali inayoonesha kuwa ombi la Mrema kweli lilipitishwa na CCM na mpinzani wake huyo aliahidiwa kazi nyingine.

Hii inaweza kuwa sababu muhimu kwa mrema kuamua kulipa fadhira kwa kukumbuka jinsi ambavyo ombi lake lilikubaliwa na chama hicho kwa namna ya kipekee.

Sababu ya pili ni ile ya ‘adui wa adui yako ni rafiki yako’. Ni dhahiri kuwa moja kati ya mahasimu wa Magufuli kisiasa hivi sasa ni mgombea ubunge wa jimbo la Vunjo kwa tiketi ya NCCR- Mageuzi, James Mbatia kwa kuwa ni mmoja kati ya washambuliaji wakuu wanaomsaidia Mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa, anayeungwa mkono na vyama vinavyounda Ukawa.

vunjo2

Mbali na kuwa mwenyekiti mwenza wa Ukawa, Mbatia ameonesha kuwa imara mara zote akipigania umoja huo. Hivyo, kisiasa, Mbatia ni adui wa Mrema na adui wa Magufuli na CCM kwa ujumla. Bila shaka hii sababu tosha ya kuwafanya hawa wawili kuwa marafiki katika kipindi hiki. Anguko la Mbatia na Ukawa ni furaha kwao wote.

Pia, Magufuli tayari ameshaweka wazi kuwa atakapokuwa rais wa Tanzania, atamtafutia Mrema kazi ya kufanya endapo hatachaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo. Hii sio tu ofa, bali Mrema anabebwa na uzoefu wake pamoja na histori nzuri ya utendaji wake hususan alipokuwa Waziri wa Mambo ya Ndani.

Kadhalika, sababu nyingine ya urafiki wa Mrema na Magufuli, ni ile iliyowekwa wazi na mwenyekiti huyo wa TLP kuwa maombi yake ya kujengewa barabara jimboni kwake yalikubaliwa na mgombea huyo wa urais ambaye pia ni Waziri wa Ujenzi.

Mrema alieleza kuwa Magufuli alipitisha ombi la mamilioni ya fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara mbalimbali jimboni kwake na hata sasa amemuahidi kumalizia baadhi ya barabara.

Hata hivyo, mtazamo wa Mrema unatofautiana na mgombea urais wa chama cha TLP, Macmillan Lyimo ambaye aliwataka watanzania kumchagua Edward Lowassa kama hawatamchagua yeye.

 

 

Messi Kusimamishwa Kizimbani
Mama Kim K Asimulia Alivyofanya Mapenzi Kwenye Ndege Halafu Mhudumu Akatangaza