Hatimaye Uongozi wa Young Africans umefichua siri ya kilichokuwa kikiendelea kati yao na Kiungo kutoka visiwani Zanzibar Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambaye bado anaendelea na msimamo wa kutoitumikia klabu hiyo.

Young Africans na Feisal Salum wapo katika mgogoro wa kimkataba, huku kiungo huyo akishinikiza mkataba wake kuvunjwa kupitia TFF, lakini Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji imeamuru suala hilo haliwezekani, zaidi ya pande hizo mbili kukaa mezani na kumalizana.

Rais wa Young Africans Injinia Hersi Said amefichua siri hiyo alipozungumza na Clouds FM mapema leo Jumatano (Mei 24) jijini Dar es salaam, ambapo amesema Fei Toto alikuwa na mahusiano mazuri na Uongozi wa Klabu, hadi kufikia kupandishiwa mshahara kutoka Milioni 1.5 hadi Milioni 4 kwa mwezi.

Injinia amesema mbali na ongezeko hilo la mshahara, pia Uongozi wa Young Africans ulimlipa Feisal Salum Shilingi Milioni 100 kama ada ya usajili ambayo ilipaswa kulipwa kwa awamu nne, lakini aliombwa alipwe kwa awamu moja ili kukidhi mahitaji yake.

“Mwaka 2020 Feisal alikuwa analipwa mshahara wa Mil 1.5 na sisi tuliboresha hadi Mil 4 na ada ya usajili Mil 100 kwa miaka minne ambayo ilikuwa apewe kwa awamu 4 lakini aliomba tumlipe yote kwa ajili ya kukidhi mahitaji yake na sisi tulifanya hivyo,”

“Feisal ni Moja ya mchezaji mzuri Katika nchi hii alipokuwa klabuni hakuwahi kuwa na tatizo lolote la kinidhamu, alikuwa akifuata taratibu zote za klabu,”

“Feisal bado anaendelea kupokea Mshaharaa Young Africans, amepokea hadi mwezi January, lakini baada ya hapo akaunti yake ilianza kuwa na shida kwa kuwa inarejesha pesa ila kila mwezi tunamuingizia pesa lakini zinarudishwa na ushahidi tunao, tumeomba akaunti mbadala ili tumuwekee pesa zake, atakapo tupa akaunti hiyo sisi tutamuingizia pesa zake zote.” amesema Injinia Hersi Said

Feisal Salum hajaitumikia Young Africans tangu mwezi Desemba mwaka 2022, na alitegemea huenda angeihama klabu hiyo wakati wa Dirisha Dogo la Usajili, lakini hatua hiyo ilishindikana baada ya kuingia katika mgogoro wa kimkataba na waajiri wake.

Tanzania kuboresha uhifadhi urithi wa ukombozi
Thierry Manzi afunguka kutua Simba SC