Watu sita wanashikiliwa na vyombo vya usalama kwa tuhuma za kupanga njama ya kufanya shambulizi dhidi ya Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron.
Watu hao ambao miongoni mwao ni wanaume watano na mwanamke mmoja, walikamatwa katika maeneo tofauti ndani ya Brittany.
Kwa mujibu wa BBC, vyombo vya usalama nchini humo vimesema kuwa kitendo cha kushughulikia makosa ya kigaidi kinaendelea kufanya upelelezi. Taarifa za kina za watuhumiwa bado hazijawekwa wazi.
“Upelelezi unalenga katika kuangalia njama ambazo hadi wakati huu zinatafsiriwa kuwa ni za shambulizi kali linalomlenga Rais Macron,” Mwendesha mashtaka alisema jana.
Tukio hilo la ukamataji limekuja katika siku ambayo Rais Macron alikuwa anatembelea maeneo ya mapigano ya Vita ya Kwanza ya Dunia, Kaskazini mwa Ufaransa.
Mwaka jana, mwanaume mwenye umri wa miaka 23 alikamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa tuhuma za kupanga njama za kumuua Rais Macron katika Maadhimisho ya Siku ya Ufaransa (Bastille Day), Julai 14.