Polisi katika jimbo la kati la Nassarawa lililopo nchini Nigeria, wamewakamata watu sita kwa tuhuma za kuendesha tovuti feki ya wapenzi wa jinsia moja ambayo huitumia kwa ajili ya kuwatapeli watu.
Watuhumiwa hao sita, walikamatwa kufuatia malalamishi ya mwathiriwa aliyedai kuwa alipigwa picha za utupu, huku kukiwa na tishio la kuzichapisha kwenye mitandao ya kijamii ikiwa hatawapatia pesa.
Kukamatwa kwa watuhumiwa hao, kunafuatiwa kuripotiwa kwa tukio hilo katika eneo la Masaka, ambalo ni la Serikali ya mtaa wa Karu, lililopo mpakani mwa mji mkuu wa nchi ya Nigeria, Abuja.
Msemaji wa Polisi wa Jimbo la kati Nassarawa, Ramhan Nansel amesema washukiwa hao ni wanaume wanne na wanawake wawili na wanadaiwa kuchapisha picha za watu wanaotaka kuwa wapenzi wa jinsia moja.
Watu hao hutumia njia za kuwalaghai wahasiriwa au kuchukua mali zao kwa nguvu na kuwafanya wanyamaze kutokana na kuhofia machapisho ya picha zao kwenye halaiki au mitandaoni.
Hata hivyo, Polisi imesema washukiwa hao watafunguliwa mashtaka baada ya uchunguzi kukamilika, ambapo katika Taifa hilo la Nigeria, mahusiano ya watu wa jinsia moja ni haramu kwa mujibu wa sheria na yeyote anayepatikana na hatia anaweza kupata kifungo cha hadi miaka 14 jela.