Hospitali ya Taifa Muhimbili imefanikiwa kupandikiza Uloto kwa wagonjwa wengine 6 na kufanya idadi ya waliopandikizwa hadi sasa kufikia 11 tangu huduma hiyo ianzishwe Novemba 2021.
Aina hiyo ya Matibabu inahusisha uvunaji, uchakataji na upandikizaji (Urejeshaji) wa chembe chembe hai mama (stemcell) za damu ambazo hutolewa kwa watu wenye magonjwa ya saratani za damu (Leukemia, multiple myeloma) na saratani inayohusisha matezi (Lymphoma). Matibabu haya hutolewa pia kwa wagonjwa wasioweza kuzalisha chembe hai za damu kama (Aplastic anaemia) pamoja na wagonjwa wa Selimundu na Thalassemia.
Naibu Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila Dkt. Julieth Magandi amesema kuwa nia ya Hospitali ya Taifa Muhimbili ni kupandikiza uloto kwa wagonjwa angalau 6 kila mwezi kwa kuwa miundombinu na wataalamu wapo tayari kufanya kazi hiyo.
“Wagonjwa wa nne kati ya sita waliopandikizwa katika awamu ya pili leo tunawaruhusu warudi nyumbani kwa kuwa afya zao tayari zimeimarika, wengine wawili bado wanaendelea na mchakato wa matibabu lakini hali zao ni nzuri” Amesema Dkt. Magandi.
Dkt. Magandi amesema weledi wa wataalamu wazalendo katika mchakato wa kupandikiza Uloto umeongezeka kwa asilimia 80 tofauti na awali ambapo ulikuwa ni asilimia 50.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Damu, Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. Stella Rwezaula amesema kuwa katika awamu hii ya pili wamepandikiza uloto kwa wagonjwa wenye tatizo la Saratani ya Matezi (Lymphoma) tofauti na awali ambapo walipandikiza kwa wagonjwa wenye saratani za damu (Leukemia, multiple myeloma) peke yake.
“Kuna tofauti kwenye kupandikiza uloto kwa watu wenye saratani ya matezi kwa kuwa wagonjwa hawa ili wapandikizwe wanahitaji maandalizi ya siku saba zaidi ya wale wenye saratani ya damu ndio maana leo tunawaruhusu wanne, wengine wawili bado tunaendelea kuwaangalia japo kuwa hali zao zinaendelea vizuri” amesema Dkt. Rwezaula
Katika hatua nyingine Dkt. Rwezaula amesema kwamba hadi sasa wananchi kutoka nchi za Kenya, Malawi na Zambia wanapiga simu kuuliza utaratibu wa wao kuweza kufika kupata huduma ya kupandikizwa Uloto.
Tanzania imekuwa nchi ya kwanza kupandikiza Uloto katika Ukanda wa wa Afrika Mashariki lakini pia nchi ya sita katika bara la Afrika.