Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda amesema kuwa asilimia kubwa ya wanawake ni aina ya watu waliokuza watoto wao katika mazingira magumu, mateso, machungu na kunyanyasika. Amesema wakina mama wamekubali kupitia hayo ili tu watoto wao wasimame na kuwa watu watakaojitegemea na kutegemewa.

Makonda amesema pamoja na hayo, kuna kundi kubwa la wauza dawa za kulevya lililodhamiria kwa makusudi kabisa kuwarudisha nyuma kwenye mategemeo yao hayo kwa ajili ya maslahi yao binafsi, amesema kundi hilo halijali kwa namna yoyote shida kubwa wanazopata wakina mama katika kuwakuza watoto wao.

Amesema kundi hilo linawaharibu watoto huku wakiwa wanajua kabisa athari kwa tamaa tu ya mali za haraka.

Makonda amezungumza hayo kupitia ukurasa wake wa ‘Instagram’ leo Machi 8, 2017 ikiwa ni siku ya Wanawake Duniani ambapo amewahakikishia wakina mama wote na wananchi wa Dar es salaam kuwa hatakubali watoto waliowabeba matumboni mwao kwa muda wa miezi tisa na kuwalea kwa tabu wafe kwa matumizi ya dawa za kulevya.

“Siku ya leo tunapoadhimisha siku ya wanawake Duniani, napenda kuchukua fursa hii kuwahakikishia kina mama wote na wananchi wa mkoa wa Dar es salaam kuwa sitakubali watoto mliowabeba matumboni mwenu miezi tisa na kuwalea kwa tabu wafe kwa matumizi ya Dawa za Kulevya” amesisitiza Makonda

Ameomba wananchi wote kuungana na Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kuhakikisha ushindi unapatikana dhidi ya wauaji na wanyonyaji wanaofanya biashara haramu ya dawa za kulevya.

“Kama uliweza kumtunza tumboni miezi tisa basi usikubali mtoto wa mwingine akakatisha matumaini yako, mlinde mwanao ili ule matunda ya uzao wako” amesema Makonda

Real Madrid Wapiga Hatua Kwa Bernardo Silva
UEFA Kuiadhibu FC Bayern Munich