Kocha mpya wa makipa wa Young Africans, Razack Siwa amesema amebaini mapungufu kwa walinda mlango wa kikosi cha klabu hiyo baada ya kuanza kazi.

Siwa alithibitishwa kuwa kocha wa makipa Young Africans mwanzoni mwa juma hili, baada ya kusaini mkataba na uongozi wa klabu hiyo ukiwasilishwa na kaimu katibu mkuu Haji Mfikirwa.

Kocha huyo kutoka nchini Kenya amesema katika mazoezi yake ya kwanza ameona udhaifu kwa makipa Metacha Mnata, Farouk Shikalo na Ramadhan Kabwili kwa asilimia 55, hivyo ana kazi ya kufanya kabla ya kuanza kwa Mshike Mshike wa Ligi Kuu April 08.

Amesema walinda mlango hao wako fiti kwa asilimia 45, na hatua hiyo ni nzuri kwake kuanza kufanya nao kazi kwa siku kadhaa zilizosalia kabla ya kucheza mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya KMC FC, mnamo April 10.

“Bahati nzuri ligi imesimama lakini kwa asilimia hizo ni vigumu sana kipa kuweza kuisaidia timu kubwa kama Young Africans kama ambavyo wengi wanatarajia,” amesema Siwa.

“Sina shaka na ubora kwa maana ya vipaji vyao, hawa ni makipa bora sana, lakini kipa ili uwe bora zaidi ni lazima uwe fiti kwa sababu ukiwa fiti unaweza kufanya uamuzi wowote mgumu katika mchezo.”

“Nimewaambia huu ni wakati wa kazi kwa asubuhi na mchana, hakuna kupumzika, najua watakuwa katika wakati mgumu lakini kama mnavyofahamu Young Africans ni klabu yenye presha kubwa, naijua, kwahiyo lazima tukimbie kutafuta mafanikio.” Amesema Kocha Siwa.

Siwa anakuwa sehemu ya benchi la ufundi la Young Africans kwa kusainidana na kocha mkuu wa muda Juma Mwambusi, baada ya uongozi wa klabu hiyo kumtimua kocha Cedric Kaze na wasaidizi wake mapema mwezi uliopita.

Waziri Ummy: TAMISEMI sio ngumu
Mwakalebela afungiwa miaka 5