Taasisi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania – SJMT na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar – SMZ zimekuwa na ushirikiano wa kuridhisha katika shughuli za kiuchumi.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamis wakati akijibu swali la Mbunge wa Baraza la Wawakilishi, Suleiman Haroub Suleiman aliyetaka kujua ni kwa kiasi gani Taasisi za SMJT na SMZ zinashirikiana katika shughuli za kiuchumi.
Amesema, pande hizo mbili zinasirikiana na katika program za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF II), Mradi wa Kuongeza Tija na Uzalishaji wa Zao la Mpunga (ERPP), Mradi wa Udhibiti Uvuvi na Maendeleo shirikishi Kusini Magharibi ya Bahari ya Hindi (SWIOFISH).
Mingine ni Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR); Mkakati wa kudhibiti Sumu Kuvu Tanzania na Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha huku akisema SJMT kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais inasimamia na kutekeleza miradi mbalimbali ya kimazingira.
“Mheshimwia Spika kuna miradi ya maabdiliko ya tabianchi inayotekelezwa Zanzibar kwa mfano hivi karibuni kama mtakumbuka tuliwahi kukabidhi boti za uvuvi Tumbatu na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar ambalo ni lengo la Serikali ya Muungano kuungano mkono uchumi buluu na suala zima la uhifahdi wa
mazingira,” amesema.
Hata hivyo, amesema kuna miradi ambayo bado haijaanza kutekelezwa ikiwemo uchimbaji wa mabwawa ya maji Bumbwini Makoba ambao tayari Serikali imetoa malekezo uanze mara moja ndani ya mwezi huu ili wananchi waanze kunufaika nao.