Halmashauri ya Wilaya Mvomero mkoani Morogoro imesema kuwa asilimia 30 kati ya asilimia 33 ya bajeti ya halmashauri hiyo inategemea mazao ya kilimo na hasa cha umwagiliaji.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, Florent Kyombo mbele ya Mkurugenzi wa Uendelezaji Miundombinu -Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Mhandisi, Senzia Maeda pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Marco Ndonde.
Wakurugenzi hao wapo wilayani Mvomero kwa lengo la kuangalia shughuli za kilimo cha umwagiliaji kinachotokana na skimu zilizopo wilayani humo ikiwa ni jitihada za Serikali kuimarisha kilimo cha umwagiliaji.
Akifafanua zaidi Kyombo amesema mchango wa kipato kinachotokana na kilimo cha umwagiliaji kwa halmashauri ni mkubwa na asilimia 33 ya bajeti ya halmashauri inategemea mazao ya kilimo na kati hizo 30 ni mazao ya umwagiliaji.
“Hivyo tukiona skimu zinaendelezwa katika Wilaya yetu na zinafanya kazi kwa ufanisi tunaamini wananchi wetu watavuna sana na maana yake hata kwa halmashauri tunatarajia mapato ya fedha za bajeti kuongezeka, hivyo kupitia fedha hizo halmashauri itajenga madarasa, zahanati, itaboresha miundombinu pamoja na kuendeleza miradi mingine ya maendeleo kwa ajili ya wananchi,”amesema Kyombo.
Pia amesema kuwa kuimarika kwa miundombinu kumekuwa kukiongeza mzunguko wa fedha, kwani sehemu kubwa ya kipato cha wananchi kinategemea kilimo na mifumo. hivyo wananchi wakivuna utaona mzunguko wa fedha unaongezeka na shughuli za uchumi zinachangamka ikiwemo watu kwenda minadani.
Akizungumzia skimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Kyombo amesema kuna skimu 11 lakini zinazofanya kazi ni chache kwani nyingine bado hazijaendelezwa.
“Ukiangalia hata maeneo yaliyowekwa miundombinu ni madogo ukilinganisha na ukubwa wa eneo la Skimu. hata hivyo kupitia skimu hizo chache ukweli ni kwamba faida zake ni nyingi sana kwani kwa sasa uzalishaji wa zao la mpunga umeongezeka na hiyo maana yake pato la mwananchi nalo limeongezeka,”ameongeza Kyombo.
Amesisitiza kutokana na kuboreshwa kwa skimu hizo wakulima wa zao la mpunga wanavuna kati ya gunia 40 hadi gunia 50 kwa ekari moja wakati huko nyuma kabla ya skimu walikuwa wnavuna kati ya gunia 10 hadi 15 tu.
Hata hivyo, ameongeza kuwa halmashauri yao nao wamejipanga ili kuwa na Skimu ambayo wanaamini itasaidia kuongeza mapato na kuwa chachu kwa wakulima wa mpunga huku akitoa rai kuwa wananchi wanalo jukumu la kuhakikisha skimu ambazo miundombinu yake imeendelezwa inalindwa. Wakati huo huo ameipongeza Serikali kwa jitihada zake za kuendeleza skimu zilizopo Mvomero kwani imekuwa ikitumia fedha nyingi kuziendeleza ikiwemo skimu ya Dakawa.