Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Miguel Angel Gamondi amesema kwa sasa Kiungo Mshambuliaji ‘Winga’ wake Mahlatsi Makudubela ‘Skudu’ hayupo kwenye mipango yake na amempa programu maalum kwa ajili ya kumuweka sawa kabla hajaanza kumtumia kwenye kikosi chake huku akisema hakuna mchezaji aliye juu ya timu.
Skudu alijiunga na Young Africans kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Mallumo Gallant ya Afrika Kusini, ambapo tangu amejiunga na timu hiyo amefanikiwa kucheza mechi moja ya kimashindano kabla ya kuumia goti ambalo lilimpelekea arejee kwao Afrika Kusini kabla ya kurudi tena nchini juma lililopita.
Gamondi amesema ameamua kumpa program maalum ya mazoezi kwa ajili ya kurudisha utimamu wake kutokana na majeraha aliyopata kabla kumjumuisha kwenye mipango yake ya michezo iliyopo mbele yake.
“Skudu amerejea na ameshajiunga na timu lakini kwa sasa amekuwa akifanya mazoezi ya pekee yake kwa sababu nimetaka afanye hivyo ili kuweza kurudisha utimamu kabla ya kumrudisha katika kundi la wachezaji wengine, najua ni mchezaji mzuri lakini siwezi kumrudisha moja kwa moja kwa kuwa ametoka kwenye majeruhi na hakuwa na timu,” amesema Gamondi na kuongeza,
“Naamini atarudisha kiwango chake na kuwa bora, ni mchezaji mzuri lakini kitu kikubwa ambacho tunaweza kuangalia kwa sasa ni wachezaji kuwa kwenye levo moja ya utimamu, ili kuweza kwenda sawa na ratiba ya mashindano yaliopo mbele yetu, wiki moja ya mazoezi ya gym naamini yatamrudisha kwenye hali yake kimwili,” amesema Gamondi.
Gamondi amesema kwenye timu yake anataka nidhamu na kujituma muda wote na hakuna mchezaji mkubwa zaidi ya timu na muda wote amekuwa akiwaambia hivyo wachezaji wake mazoezini na hata kwenye kambi yao.