Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Afrika Kusini aliyesajiliwa na Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Mahlatse Makudebela ‘Skudu’, amesema anataka kuwaona Simba SC ili afahamu ubora wao.
Mchezaji huyo ambaye ni mchezaji wa kwanza raia wa Afrika Kusini kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara amepokelewa kwa shangwe kubwa na mashabiki wa Young Africans katika utambulisho wa wachezaji kwenye tamasha la klabu hiyo lililofanyika mwishoni mwa juma lililopita.
Kwenye Wiki ya Mwananchi, Skudu alicheza kwa dakika 45 dhidi ya Kaizer Chiefs lakini aliwashawishi mashabiki kwa kuuchezea mpira kwa ustadi wa hali ya juu.
Skudu amesema kuwa licha ya mashabiki kumpokea kwa shangwe lakini bado ana kazi kubwa ya kujituma ili kupata nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha Kocha Miguel Gamondi huku pia akisubiri kuona ubora wa Simba SC.
Amesema Young Africans ni timu kubwa na ina wachezaji bora hivyo pamoja na umaarufu alionao na upendo waliouonyesha mashabiki lakini kazi kubwa ni kupata namba uwanjani.
“Nasubiri kuwaona Simba SC na Azam FC ili nijue wana ubora kiasi gani, lakini kwa ujumla lazima nikuhakikishie kuwa tuna timu bora.
“Ni kazi kubwa kupata namba hapa kwani wachezaji wengi wako vizuri na wanahitaji nafasi ya kucheza, hivyo mtihani mkubwa ni kuonyesha uwezo kwenye kila mchezo,” amesema mchezaji huyo aliyejiunga na Young Africans akitokea Marumo Gallats ya Sauzi na kuongeza:
“Tumekuja kuipa timu mafanikio na kitakachotupa nguvu ni ushirikiano, lakini natakiwa kuonyesha juhudi za hali ya juu kama nataka kucheza.”