Kiungo Mshambuliaji wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans, Mahlatsi Makudubela ‘Skudu’, leo Jumanne (Agosti 15) anatarajiwa kuanza mazoezi na wenzie baada ya kupona majeraha aliyoyapata katika mchezo wa nusu fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC.

Skudu aliumia goti la mguu wa kushoto katika mchezo huo uliochezwa wiki iliyopita katika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga ambao Young Africans ilishinda mabao 2-0.

Nyota huyo raia wa Afrika Kusini alitolewa uwanjani dakika ya sita ya mchezo huo baada ya kuchezewa rafu na James Akamiko na nafasi yake kuchukuliwa na Chrispin Ngushi.

Daktari wa Young Africans, Moses Etutu, amesema Skudu alipatwa na maumivu makali hali ambayo walilazimika kwenda hospitali baada mchezo kumalizika.

Amesema walimpeleka hospitali mchezaji huyo na kufanyiwa vipimo lakini bahati nzuri alionekana hajavunjika hivyo wakaruhusiwa kurudi naye kambini.

“Kwa sasa anaendelea vizuri, leo ataanza mazoezi na wenzake baada ya kumaliza programu yake pekee yake na kuinekana yupo fiti,” amesema.

Staa huyo ambaye anatumia mguu wa kushoto, anasubiriwa kwa hamu na mashabiki wa timu hiyo ambao wanaamini atakuwa msaada mkubwa katika kikosi cha timu hiyo katika msimu wa 2023/2024.

Skudu aliyejiunga na Young Africans kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Marumo Galants ya Afrika Kusini, amewahi kupita katika klabu za Orlando Pirates, Chippa United, Platinum Stars na nyingine.

Hasheem Ibwe: Endeleeni kuibeza Azam FC
Gamondi aufurahisha uongozi Young Africans