Shirika la kimataifa lisilo la kiserikali la Sightsavers limekabidhi vifaa vyenye thamani ya shilingi 78,765,898 kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili visaidie katika kuboresha huduma za macho na kutokomeza upofu unaoweza kutibika.
Vifaa hivyo vimekabidhiwa hivi karibuni Mjini Unguja na Mkurugenzi wa Shirika hilo, Gosbert Katunzi ambaye amesema msaada huo ni mwendelezo wa mkakati wa shirika hilo kusaidia juhudi za Serikali katika kuinua huduma za Afya.
Katunzi amesema tangu mwaka 2012-2016 jumla ya shilingi bilioni 1.6 zimetumika katika kutoa misaada kwenye sekta ya afya ambapo vifaa pekee vimegharimu jumla ya kiasi cha shilingi 309,419,399.
Pia jumla ya shilingi bilioni 1.3 zimetumika katika kukarabati majengo ya matibabu ya macho katika Hospitali za Mnazi Mmoja, Wete na Chakechake Vision Centre, kusomesha wataalam wa macho wa kada mbalimbali, manunuzi ya dawa, kufanya uhamasishaji jamii pamoja na kuwezesha huduma karibu na wananchi.
“Katika kipindi cha miaka mitano wananchi takribani 1,065,060 wamenufaika na huduma za uchunguzi wa macho ambapo kati ya wananchi 4,307 waliofanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho watoto ni 408, waliopatiwa miwani ni 18,529 na waliopatiwa matibabu mengine ya macho ni 300,640,” amesema Katunzi.
Aidha, Katunzi amevitaja baadhi ya vifaa vilivyotolewa na taasisi yake kuwa ni kifaa cha kuchunguza saratani ya macho pamoja na vifaa vya uchunguzi wa macho(uoni) kiujumla pamoja na lensi mbalimbali za kutengenezea miwani ya watoto na watu wazima.
Vile vile, Katunzi amewashukuru Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mahmoud Thabit Kombo pamoja na watendaji wa Wizara yake kwa kudumisha ushirikiano na taasisi yake pamoja na wadau mbalimbali wa afya katika kuhakikisha wananchi wa visiwani wanafikiwa na huduma za afya.
Hata hivyo, Shirika la Sightsavers ni shirika la kimataifa lisilo la kiserikali linalofanya kazi kwa ushirikiano wa nchi zinazoendelea katika kuzuia upofu unaozuilika, pamoja na kusaidia wagonjwa wa macho wenye uoni hafifu na ulemavu unaotokana na magonjwa ya macho, Sightsavers ilianza kufanya kazi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tangu mwaka 2006.