Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, imesema kuwa kukamilika kwa Uwanja wa michezo wa Amaan kisiwani Unguja, kutatoa kutoa fursa kwa nchi zenye uhitaji kuutumia.
Hayo yamesemwa na Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah, alipofanya ziara ya kutembelea uwanjani hapo, kukagua maendeleo ya ujenzi wa uwanja huo ambao upo katika hatua za mwisho.
Abdullah amesema kwa kuwa uwanja huo ni wa kisasa, una viwango vya kimataifa, nchi zenye uhitaji zinaweza kuwasiliana na Serikali na kupewa fursa ya kuutumia.
Makamu huyo wa Rais alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussen Ali Mwinyi, kwa kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar, kwa kuamua kuujenga upya Uwanja wa Amaan kwa lengo la kuwawezesha wanamichezo wa Zanzibar, nje ya Zanzibar kucheza katika kiwanja chenye mandhari nzuri na hadhi ya kimataifa.
Amesema serikali ina imani kubwa na kampuni ya ORKUN inayojenga uwanja huo na kuutaka uongozi wa kampuni hiyo kukamilisha ujenzi kwa wakati na kiwango kilichokusudiwa, kwa maslahi ya wananchi na taifa kwa ujumla.
Ameongeza kuwa, wakandarasi na mshauri elekezi wa mradi wanapaswa kuongeza kasi ya ujenzi kwa kufanya kazi usiku na mchana, kwa uwaminifu lengo likiwa kukamilisha ujenzi kwa wakati.
“Ujenzi wa uwanja huu ni utekelezaji wa llani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), inayowataka viongozi kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, zinazoendana na wakati ikiwemo michezo.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni na Michezo, Fatma Hamad Rajab, amesema Uwanja wa Amaan umejengwa kwa kuzingatia viwango kimataifa, matakwa ya Shirikisho la Soka Duniani ‘FIFA’.
Fatma amesema uwanja huo unatarajiwa kuchukua watazamaji 16,000 na kutoa fursa kwa timu za ndani na nje ya nchi kuutumia.
Pia, amesema uwanja huo unajumuisha viwanja vingine vikiwemo vya Netiboli, Mpira wa Wavu, Mpira wa Mikono, Ukumbi wa Judo, michezo ya ndani (Indoor).