Kiungo mpya wa Manchester United, Sofyan Amrabat yupo fiti na amejumuishwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Morocco kwa ajili ya mechi za kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
Taarifa ya awali zilidai kiungo huyo vipimo vyake viligundulika kuwa ana tatizo la mgongo kama Mshambuliaji mpya Rasmus Hojlund wakati anajiunga akitokea Atalanta.
Jambo hilo lilizua taharuki kwa mashabiki, lakini imeripotiwa kwamba kiungo huyo hatakuwa nje ya uwanja kwa wiki sita kama ilivyoelezwa siku chache baada ya kutambulishwa.
Kwa mujibu wa taarifa, Amrabat aliwasili Manchester akiwa na tatizo la mgongo na iligundulika baada ya kufanyiwa vipimo vya afya.
Mchezaji huyo alikamilisha uhamisho wa kujiunga na Man United kwa mkopo akitokea Fiorentina huku kukiwa na kipengele cha kununuliwa jumla itakapofika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Kiungo huyo aliweka picha yake akiwa Carrington katika akaunti ya Instagram baada ya kutambulishwa na klabu hiyo na alikosa mechi dhidi ya Arsenal mwishoni mwa juma lililopita kwa sababu alichelewa kuripoti, lakini mchezaji mwingine aliyesajiliwa kwa mkopo Sergio Reguilon alijumuishwa kwenye kikosi ingawa hakucheza.
Beki huyo wa kimataifa wa Hispania, Reguilon alijiunga kwa mkopo akitokea Tottenham Hot spur ambapo naye alitupia picha mtandaoni akiwa na uzi wa Mashetani Wekundu kupitia akaunti yake ya lnstagram.