Mpango wa Mashabiki wa klabu ya Young Africans wa kumpokea mshambuliaji kutoka Burkina Fasso, Yacouba Sogne Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere, umegonga mwamba, kufuatia mchezaji huyo kushindwa kuwasili kwa wakati.

Young Africans imemsajili mshambuliaji huyo wa zamani wa Asante Kotoko ya Ghana kwa mkataba wa miaka miwili na alitarajiwa kutua leo saa 7 mchana lakini badae ikawa tofauti na viongozi wakieleza kwamba kumetokea mabadiliko ya ndege na atalazimika kuwasili usiku.

Mashabiki walifika tangu saa 4:00 asubuhi kumpokea Sogne, baada ya kufika saa 7:00 mchana wakaanza kuwasiliana na viongozi wao wa matawi na ndipo walipogundua kwamba ratiba yake imebadilika wakaanza kusepa.

Pamoja na baadhi yao kwenda kuuliza kwa wahudumu wa eneo hilo kama wana taarifa za mchezaji kutua muda huo na ndege kutoka Ethiopia, walijibiwa hakuna suala kama hilo.

“Ni kweli alikuwa awasili mchana huu lakini kumetokea mabadiliko ya ndege, hivyo atawasili usiku,”Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli amesema .

Polisi waliamua kuingilia kati kwenda kuzungumza nao na kuwataka wafanye mawasiliano vizuri na viongozi wao ili wajue muda sahihi warudi badae.

“Jamani tunawaomba muende kwasababu mmeshajihakikishia mchezaji wenu haji leo, hivyo ni bora mkaendelee na majukumu yenu,”

“Hapa ni eneo ambalo kila mtu ana uhuru wakuwepo, ndio maana tunawashauri kwa amani ili mkaendelee kulijenga Taifa katika maeneo ama shughuli tofauti, ukweli mmeupata kama mtaelewa basi maamuzi mnayo wenyewe,” walisema Polisi

Hata hivyo mashabiki walikuwa kama hawajaelewa kwani waliendelea kupiga kambi eneo hilo, kama dakika 15 hivi kisha wakaanza kuondoka mmoja mmoja.

Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo kongwe katika ukanda wa Afrika Mashariki na kati, wamekua na utamaduni wa kufanya mapokezi kwa wachezaji waliosajili kaytika kipindi hiki cha kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ambapo wameshafanya hivyo kwa wachezjai kutoka DR Congo Tuisila Kisinda na Mkoko Tonombe, Michael Sarpong kutoka Ghana na Carlinhos kutoka Angola.

TCAA yatoa sababu Ndege za Kenya kuzuiwa
Rungu la TCRA laishukia Clouds Media