Saa kadhaa baada ya kukamilisha mipango ya usajili wa kujiunga na klabu ya Villareal ya nchini kwao Hispania, mshambuliaji Roberto Soldado ametoboa siri ya kushindwa kuwika katika ligi ya nchini England akiwa na klabu ya Tottenham Hotspurs.

Soldado, amelazimika kurejea nyumbani baada ya uongozi wa Villareal kuafiki mpango wa kumsajili kwa ada ya uhamisho wa paund million 7 akitokea White Hart Lane.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 30, amesema ilikua ni vigumu kwake kuwika katika ligi ya ugenini tofauti na ilivyokua nyumbani wakati alipokua na klabu ya Valencia kutokana na mazingira yaliyokua yakimzunguuka.

Soldado amesema wakati mwingine alikua anahisi kama amefungwa na kujikuta akishindwa kufanya maamuzi sahihi alipopata nafasi ya kuchezeshwa na wengine uwanjani, hali ambayo ilimnyima fursa ya kujiamini.

Amesema dhamira yake ilikua ni kuonyesha kiwango kikubwa akiwa nje ya nyumbani kwao Hispania, lakini alijikuta anaifungia Spurs mabao 16 pekee, katika michezo 76 aliyocheza tangu mwaka 2013.

Soldado alijiunga na Tottenham kwa ada ya uhamisho wa paund million 26 na alitarajiwa kuwa na makali hasa baada ya klabu hiyo kukubali kumuachia Gareth Bale ambaye alielekea Real Madrid kwa ada ya usajili iliyovunja rekodi dunaini.

Soldado jana alitambulishwa rasmi mbele ya waandishi wa habari na amekabidhiwa jezi namba tisa huku akipewa nafasi kubwa ya kuwa sehemu ya kikosi cha Villareal ambacho kitaanza msimu mpya wa ligi mwishoni mwa juma hili kwa kupambana na Real Betis.

Everton Kusajili Beki Kisiki Kutoka River Plate
Esther Bulaya Haepukiki Bunda, Wassira Kugawanya Nguvu