Mshambuliaji kutoka Korea Kusini na klabu ya Tottenham Hotpur, Son Heung-Min, ametangaza nia yake ya kubakia klabuni hapo licha ya kupokea ofa nono ya kujiunga na klabu ya Saudi Arabia, Al Ittihad.
Mwanzoni mwa juma hili ESPN ilifichua kwamba mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30 amekuwa akilengwa na Klabu za Saudia huku Al Ittihad ikimpa fowadi huyo ofa ya mkataba wa miaka minne wenye thamani ya euro milioni 30 kwa msimu.
Chanzo kilicho karibu na mazungumzo kilidokeza kuwa upande wa Saudia ulikuwa unaandaa dau la ufunguzi la euro milioni 60 pamoja na bonasi, lakini Tottenham walisema hawakutaka kusikiliza ofa za fowadi huyo raia wa Korea Kusini.
Akizungumza Jumanne, Son aliamua kuzima uvumi juu ya uhamisho kwa kusisitiza kujitolea kwake kwa Spurs.
Son amenukuliwa na ripota wa soka wa Korea, Sungmo Lee akisema: “Nina mambo mengi ya kufanya katika Ligi Kuu.
Fedha haijalishi kwangu sasa, na fahari ya kucheza soka, kucheza ligi ninayoipenda ni muhimu, nataka kuichezea Tottenham zaidi kwenye Ligi Kuu. Nitajiandaa vyema nitakaporejea Spurs.”
Chanzo hicho kilidokeza kuwa kulikuwa na matumaini kwamba Son anaweza kujaribiwa kuhamia Al Ittihad kutokana na klabu hiyo kuwa tayari imekubali dili la kumsajili mshambuliaji wa Ufaransa.
Karim Benzema, huku kiungo wa Chelsea, N’Golo Kante akiwa tayari ametambulishwa juzi Mkataba wa sasa wa Son na Tottenham unamalizika mwaka 2025.