Licha ya timu yake kuwa na faida ya ushindi wa bao 1-0 ilioupata nyumbani, mshambuliaji wa FC Platinum, Silas Songani amesema kuwa wana kazi kubwa ya kufanya ili kuitupa nje Simba kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Songani hakucheza katika mchezo wa mkondo wa kwanza jijini Harare kutokana na majeraha, ni miongoni mwa nyota 23 walio katika msafara wa timu hiyo ambao uliwasili nchini juzi Jumamosi (Januari 02), tayari kwa mchezo mkondo wa pili dhidi ya Simba utakaochezwa kuanzia saa 11 jioni katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini.

Songani amesema licha ya timu yake kuwa na faida ya ushindi wa nyumbani, katika mchezo wa mkondo wa pili keshokutwa Jumatano wanahitajika kupambana kwa hali na mali.

“Tulipata matokeo mazuri dhidi ya Simba  lakini fundo moja halitoshi kusaidia kwenye kiangazi. Tunatakiwa kuwamaliza Simba.”

“Tuna kazi kubwa mbele yetu lakini uaminifu, uadilifu, kujituma na utayari wa kusonga mbele ni chachu kwetu kusonga mbele.”

“Kinachonivutia zaidi kwa hili kundi ni kiu ya kufanya mazoezi kwa bidii na kila mchezaji anapambana ili apate nafasi kwenye timu,” amesema Songani.

Mshambuliaji huyo pia ameushukuru uongozi wa FC Platinum kwa kuisafirisha timu mapema kuja Tanzania ili kuwawezesha wachezaji kuzoea hali ya hewa ya jiji la Dar es Salaam.

Katika mazoezi ya kwanza ya FC Platinum, kiwango cha joto kilikuwa ni nyuzi 31 wakati kiwango cha unyevu kilikuwa ni asilimia 66.

FC Platinum wanahitaji matokeo ya ushindi au sare ya aina yoyote ili wasonge mbele lakini hata wakipoteza mchezo kwa utofauti wa bao moja huku wakiwa wamefumania nyavu, watajihakikishia kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya tatu mfululizo.

Timu yoyote inayotinga hatua hiyo ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, inakuwa imejihakikishia kitita cha Dola 550,000 (zaidi ya Sh 1.2 bilioni), kiasi ambacho kinaweza kuongezeka ikiwa itasonga mbele katika hatua zinazofuata.

Zidane akataa kumpumzisha Benzema
Pelosi achaguliwa tena Uspika Bunge la Marekani