Ikiwa imesalia michezo miwili Ligi ya Championship kufikia tamati, huku JKT Tanzania ikifanikiwa kurejea Ligi Kuu msimu ujao, vita ya ufungaji bado inaendelea.

Edward Songo, mfungaji wa JKT Tanzania ameandika rekodi mbili ndani ya ligi hiyo huku akibakiza rekodi moja ya kuibuka mfungaji bora kwa mara nyingine.

Songo ambaye ni mfungaji bora wa msimu uliopita kwa mabao yake 15 alikuwa mfungaji wa kwanza ndani ya misimu mitano kuwa mfungaji bora halafu timu yake haikupanda Ligi Kuu.

Rekodi ya kwanza aliyoweka msimu huu ni kuvunja rekodi yake mwenyewe aliyoweka msimu uliopita kwani hadi sasa amefunga mabao 18, na anawania kuwa mfungaji bora mara ya pili mfululizo.

Rekodi ya pili aliyoiweka mchana nyavu huyo ni kuvunja rekodi ya mabao mengi ambayo ilidumu tangu msimu wa mwaka 2017/18 iliyowekwa na mchezaji wa timu ya JKT Tanzania, Hassan Mwaterema kwa kufunga mabao 16.

Hata hivyo msimu wa 2018/19, Reliants Lusajo (Namungo) naye alifunga mabao 16 lakini rekodi ikabaki ya Mwaterema ambaye alikuwa wa kwanza kuiweka.

Msimu wa 2019/20, Anuary Jabiry (Dodoma Jiji) aliibuka kinara wa mabao 10 huku William 2020/21 Edgar (Mbeya Kwanza) akifunga mabao 13 na misimu hiyo yote timu zao zilipanda daraja kwenda Ligi Kuu.

Msimu uliopita licha ya Songo kuwa mfungaji bora lakini waliendelea kusota Championship ambapo sasa maafande hao ndio wamefanikiwa kurejea Ligi Kuu baada ya misimu miwili kupita.

Songo alisema imekuwa faraja kubwa kwake kuendelea kuaminiwa na benchi la ufundi linaloongozwa na kocha Malale Hamsini sababu kocha aliyewaongoza msimu uliopita na sasa ni tofauti.

Liverpool kujaribu tena kwa Jude Bellingham
Usajili Man Utd 2023/24 kufuru